2013-01-28 08:54:16

Liturujia ya Kanisa ni shule ya kumsikiliza Mwenyezi Mungu!


Marafiki wa Mungu ni wale ambao wanajifungua mbele ya Mungu na kujibidisha kuifahamu Injili. Yesu alijitahidi kushiriki katika Liturujia ya watu wake kwa njia ya Sala na Tafakari ya Torati na kwamba, uwepo wake kati yao ni kielelezo cha utimilifu wa utabiri uliokuwa umetolewa na Manabii katika Maandiko Matakatifu.

Roho wa Bwana yu juu yake amempaka mafuta kuwahubiria maskini Habari Njema, changamoto kwa waamini na wote wenye mapenzi mema kumsikiliza kwa makini na kumwamini, kwani ndiye Mkombozi wa dunia aliyezaliwa kwa ajili yao kule mjini Bethlehemu.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa tafakari yake kwa mahujaji na waamini waliokuwa wamekusanyika kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, hapo tarehe 27 Januari 2013.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusherehekea Jumapili ambayo kimsingi ni Siku ya Bwana, kwa kuitumia kwa ajili ya mapumziko ya kifamilia; kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; linalowakirimia waamini Mkate wa uzima wa milele na Neno la Mungu ambalo ni taa inayoangaza miguu yao.

Ni mwaliko wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu linalotangazwa, kwani hiki ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Liturujia ya Neno la Mungu ni shule ya kumsikiliza Mungu anayeongea na watu wake kutoka katika undani wa maisha yao! Waamini watumie fursa mbali mbali ili waweze kutubu na kuongoka, kwani kazi ya ukombozi anasema Baba Mtakatifu ni mchakato endelevu katika historia ya Kanisa na maisha ya kila mwanadamu. Huu ndio wakati ambao Mwenyezi Mungu anamwalika mwanadamu ili aweze kumkirimia wokovu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha kuiga ili kutambua alama za uwepo wa Mungu nyakati zote katika maisha ya kila mwanadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.