Juma la kuhamasisha miito ya kitawa ndani ya Kanisa nchini Ureno
Mahujaji wa Imani, mitume wa Uinjilishaji Mpya ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho
ya Juma la Kuombea Miito Mitakatifu nchini Ureno, linaloanza hapo tarehe 27 Januari
hadi tarehe 3 Februari 2013.
Maaskofu Katoliki
nchini Ureno wanabainisha kwamba, kwa namna ya pekee, watawa ni mahujaji wa imani,
mitume wenye nguvu na uzuri wa imani ni watu wanaosukumwa na upendo wa Kristo ili
kujitoa kimaso maso kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji, sehemu mbali mbali za dunia.
Hii ni dhamana kwa Wakristo wote waliobatizwa ndani ya Kanisa, lakini, ni
changamoto ya pekee inayofanyiwa kazi na watawa katika maisha yao ya kila siku, kwa
kumfuasa Kristo katika maisha ya utii, ufukara na usafi kamili. Hiki ni kielelezo
cha neema na ushuhuda unaoonesha muungano wao wa karibu na Mwenyezi Mungu. Itakumbukwa
kwamba, imani ya kweli ni jibu endelevu linaloonesha katika uhalisia wa maisha, ile
nguvu inayotenda kazi ndani mwao; nguvu ambayo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na
sita anasema, inapaswa kukua na kukomaa, ili kutoa matunda yanayokusudiwa, yaani wongofu
na utakatifu wa maisha.
Imani tendaji anasema Baba Mtakatifu inajionesha hata
katika vipaumbele vya maisha ya waamini, lakini kwa watawa, imani hii ni kielelezo
cha mikakati ya huduma inayotolewa na Mama Kanisa kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, kutokana na hali yao ya maisha. Ni imani inayobubujika katika
maisha ya watawa kwa kukutana na Yesu Kristo aliyeuabadili maisha na vipaumbele vyao.
Ni Makatekista wa kwanza wa Imani, wanaojitoa kila siku, kurithisha imani
hii kwa watoto na vijana wanaofanya hija ya kumtafuta, kumfahamu ili hatimye, kumpenda
na kumtumikia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
Watawa ni kielelezo cha imani
inayoungamwa na Mama Kanisa, Imani ambayo inaadhimishwa katika Mafumbo ya Kanisa,
kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa zinazomkirimia
mwamini baraka na neema anazohitaji katika hija yake ya Imani. Kwa namna ya pekee,
hii ni Imani inayojidhihirisha katika maisha ambayo yanaoongozwa na Amri za Mungu,
ili kumwezesha mwamini kuwa adili katika maneno na matendo yake. Mwishoni, hii ni
Imani inayomwilishwa katika Sala.
Watawa ni mashahidi hai wa Injili ambayo
inamwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuonesha uzuri na nguvu ya imani tendaji
katika maisha ya mwamini. Ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, linawaalika
Watawa kwa namna ya pekee, kukumbatia Fumbo la Imani, sababu maalum ya wito na maisha
yao, changamoto ya kuendeleza utume wa Kanisa unaojikita katika Uinjilishaji Mpya,
kwa kusoma alama za nyakati, kwa kutambua kwamba, hata Wakristo wengine wanashiriki
dhamana hii, lakini kwa kiwango tofauti.
Maaskofu wanasema, Waamini wanaweza
kuendelea kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya Sala endelevu; Katekesi ya
kina; elimu ya dini shuleni, kwa kumwilisha Injili katika matendo ya huruma pamoja
na kujitoa kimaso maso kuwatangazia Injili wale ambao bado hawajabahatika kusikia
Injili ya Kristo ikitangazwa katika viunga vyao.
Kiungo makini katika kutangaza
Imani ni ushuhuda unaotolewa na waamini wote kila mtu kadiri ya maisha na wito wake
ndani ya Kanisa. Ni mwaliko wa kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya tunu
msingi za Kiinjili, Maadili na Utu wema, kwani kuna hatari kubwa kwamba, watu wengi
wakaendelea kumezwa na malimwengu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno, linawashukuru
na kuwapongeza Watawa wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume wanaofanya kazi zao
ndani na nje ya Ureno kwa ushuhuda makini na endelevu wanaoutoa kwa maisha na utume
wa Kanisa.