2013-01-26 09:14:57

Mshikamano wa umoja na upendo miongoni mwa waamini Marekani na Amerika ya Kusini


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, linawaalika waamini na wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kukusanya matoleo kwa ajili ya kusaidia kuenzi mshikamano wa upendo na Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini, kama njia ya kuwahamaisha kutolea ushuhuda imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kuanzia tarehe 26 Januari hadi tarehe 27 Januari 2013, waamini watakusanya fedha kwa ajili ya kugharimia miradi mbali mbali inayotekelezwa na Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini na katika nchi za Caribbean.

Miradi inayokusudiwa kwa Mwaka 2013 ni ile inayogusa shughuli za Uinjilishaji, majiundo kwa viongozi wa Kanisa pamoja na kuwajengea Makatekista uwezo wa kufundisha: Imani, Sakramenti, Neno la Mungu na Maisha ya Sala. Fedha hii pia inalenga kusaidia juhudi za malezi kwa Majandokasisi na Watawa katika nyumba za malezi. Kwa njia hii, Kanisa Katoliki nchini Marekani, linashirikisha furaha ile inayobubujika kutoka katika visima vya imani kwa watu wanaoishi Amerika ya Kusini na katika nchi za Caribbean.

Maaskofu Katoliki Marekani wanasema kuwa, mchango huu ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa dhati na shukrani kwa waamini ambao wanatoka katika nchi hizi na kwa sasa wanayo nafasi nzuri ya maisha na uchumi, kuendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya jirani zao, ambao bado wanaendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.

Katika kipindi cha Mwaka 2012, kiasi cha dolla za kimarekani million 6.5 zilitolewa kama msaada ili kugharimia miradi 417 iliyokuwa imepewa kipaumbele cha kwanza kwa Mwaka 2012. Kiasi hiki cha fedha pia kilitumika kwa ajili ya kugharimia ukarabati wa Makanisa yaliyokuwa yamebomeolewa kutokana na majanga asilia katika nchi za Amerika ya Kusini, kwa namna ya pekee, Cuba na Haiti.








All the contents on this site are copyrighted ©.