2013-01-26 10:07:54

Hali ya wananchi wa Mali bado ni tete!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hivi karibuni alirudia tena kutoa wito wake kuhusu kusitisha vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia na kuwataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na ujasiri wa kuanzisha mchakato wa majadiliano yatakayosaidia kudumisha misingi ya haki na amani.

Kutokana na changamoto hii inayojitokeza kwa namna ya pekee katika Ukanda wa Sahel ambao kwa sasa unakabiliwa na vita inayoendelea hasa nchini Mali, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Italia, Caritas Italia, linasema, litaendelea kutoa huduma ya msaada wa kibinadamu kwa waathirika wa vita nchini Mali, huku nao pia wakiendelea kuhimiza umuhimu wa kujikita katika majadiliano.

Taarifa zinabainisha kwamba, katika Ukanda wa Sahel unaoziunganisha nchi za Burkina Faso, Niger, Mauritania na Mali, Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Mali na Burkina Faso yanaendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa wakimbizi 45, 000 ambao wanahitaji pamoja na mambo mengine: chakula, maji, mahema, mablanketi pamoja na huduma za afya. Idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na watu kuhofia maisha yao. Kuna zaidi ya watu 400,000 hawana makazi ya kudumu na wanaendelea kutafuta hifadhi katika nchi jirani. Kama hali ya utulivu na usalama haitaweza kufikiwa mapema, kuna hatari kwamba, idadi ya wakimbizi ikaongezeka maradufu!







All the contents on this site are copyrighted ©.