2013-01-26 13:23:00

Hali ya ulinzi, usalama na amani Barani Afrika bado inachechemea!


Bara la Afrika linaendelea kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama kutokana na kinzani za kisiasa na migogoro ya kivita inayoendelea kusikika sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, licha ya kuwa na matumaini ya kumalizika kwa hadha hizi kwa njia ya majadiliano. Ni mwaliko kwa Serikali za Umoja wa Afrika kutafuta na hatimaye kutibu vyanzo vya kinzani na migogoro hii inayopelekea watu wasiokuwa na hatia kuendelea kupoteza maisha na mali zao.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Dr. Nkosazana Dlamini Zuma, Kamishina wa Umoja wa Afrika, wakati wa kufungua mkutano wa Baraza la amani na usalama na Umoja wa Afrika, hapo tarehe 25 Januari 2013. Bara la Afrika linaendelea kuwekeza katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu kati ya Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini kwa kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa katika hatua mbali mbali zilizosimamiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Hali ya ulinzi na usalama nchini Mali bado ni tete na Umoja wa Afrika unafuatilia hali hiyo kwa umakini mkubwa, kutokana na ukweli kwamba, Mali ni eneo la hatari kwa usalama na amani kwa Umoja wa Afrika, kutokana uwepo wa makundi ya kigaidi, wanajeshi waasi na watu wanaojihusisha na vitengo vya jinai. Umoja wa Afrika unaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupambana na vitendo vyote hivi ili kuweza kurejesha amani na utulivu Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.