Sikuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, mtume na Mwalimu wa Mataifa: kutembea katika
furaha na sherehe
Katika siku hii ya nane na ya mwisho ya kuombea Umoja wa Wakristo, wazo letu kuu ni
kutembea katika furaha na sherehe. Kwenda kwa unyenyekevu
na Mungu maana yake kutembea katika furaha na sherehe. Mtu anayewatembelea wenye shida
na dhiki anakutana nao katika furaha na dhiki zao. Mfano mzuri ni wa wale walio na
matatizo mazito ya umilikaji wa ardhi, wasiokuwa na makazi na kazi. Hata katika
masomo ya leo tunaona ujumbe wa matumaini na sherehe Nabii Habakuki anafurahi katika
Bwana wakati wa ukame na njaa. Ushuhuda ya kwamba Mungu atakuwa pamoja na watu wake
katika matatizo yao ni sherehe ya matumaini. Bikira Maria anamtembelea binamu yake
Elizabet kufurahi naye katika ujauzito wake. Anaimba ”Magnificat”, utenzi
wake wa kumtukuza Mungu, utenzi wenye matumaini hata kabla mtoto wake hajazaliwa.
Kutoka gerezani, Mtakatifu Paulo Mtume kwa Mataifa anazihimiza Jumuia za Kikristo
zilizoko Filipi kufurahi na kusherehekea akisema: Furahini katika Bwana siku zote.
Katika Biblia, sherehe na furaha inahusishwa na matumaini katika uaminifu wa Mungu.
Tunaposali kuomba umoja wa Wakristo wiki hii, tukiwa katika siku ya mwisho, tukiiombea
kwa namna ya pekee wakati huu Jumuia ya Wadalit kule India, tujiangalie, tujichunguze
pia sisi wenyewe juu ya utambuliko wa hali yetu ya kikikristu katika njia ya imani. Sherehe
na furaha yetu ya kuwa na umoja miongoni mwetu sisi wakristo bado lazima ipokelewe
katika matumaini na mapambano. Imejikita katika matumaini kwamba Sala ya Kristo ili
tuwe wamoja itatekelewa katika muda wa kimungu na kupitia njia za kimungu. Ina msingi
katika shukrani kwamba umoja ni zawadi ya Mungu na katika kutambua kwamba umoja tulio
nao kama marafiki wa Yesu ni ule unaoonekana katika ubatizo. Imejisimika katika
imani kwamba, Mungu anamwita kila mmoja wetu kufanya kazi kuleta umoja na kwamba juhudi
zetu zitatumiwa na Mungu, tukimuamini Mtakatifu Paulo anayetuambia, katika kila katika
Sala na shukrani maombi yenu yajulikane kwa Mungu. Kutembea na Mungu kuelekea umoja
wa kanisa kunatuhitaji tutembee kinyenyekevu na Mungu katika sherehe na furaha, katika
sala na matumaini.
SALA Ee mungu wa rehema, tunaomba roho wako mtakatifu
azijaze jumuia zetu furaha na sherehe ili tuweze kuufikia umoja tunaoushiriki tayari
na kuendelea kwa bidii moja kuutafuta umoja unaoonekana. Tunafurahi katika imani na
matumaini kwa jina la wale wote wanaokataa heshima yao kupungua, tukiona ndani yao
neema na ahadi ya uhuru. Tunaomba utufundishe kushiriki furaha na kujifunza kutokana
na uvumilivu wao. Washa tena ndani yetu matumaini na tegemeza maazimio yetu, ili kwa
jina la yesu Kristu tuweze kutembea pamoja katika upendo, tukiinua sauti ya pamoja
kwa upendo, tukiimba kwa pamoja kukuabudu. Mungu wa uzima tuongoze katika njia ya
haki na amani. Amina. MASWALI Ni mapambano gani kuelekea kwenye haki yapo katika
jumuia yako? Ni nini chanzo cha kusherehekea? Ni mapambano gani kuelekea Umoja
wa Wakristo yapo katika jamii yako? Je, chanzo cha kusherehekea ni kipi ? Tafakari
hii imeandaliwa na Padre Emmanuel Nyaumba.