2013-01-23 09:00:07

Uchaguzi mkuu Kenya: Shabikia Amani na Kura yako!


Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Vyama vya michezo, wadau na wapenda amani nchini Kenya; kwa pamoja wamezindua kampeni inayoongozwa na kauli mbiu "Shabikia Amani na Kura yako" inayowahamasisha wananchi nchini Kenya kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi, huku wakizingatia misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, vurugu na kinzani zilizojitokeza mara baada ya uchaguzi mkuu nchini humo katika miaka ya 1992, 1997 na ule wa mwaka 2007 uliopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na vurugu. Kampeni hii inavihusisha vyama mbali mbali vya michezo nchini Kenya, kwani huko kuna wanachama wengi na ujumbe unaweza kufika kwa urahisi.

Vyombo vya mawasiliano ya Jamii vinahamasishwa pia kusaidia kuwajengea wananchi uwezo kukua na kukomaa katika masuala ya kidemokrasia, kwa kuheshimu na kuthamini uhuru na haki msingi za binadamu. Wanasiasa washindane kwa sera, nidhamu na uwajibikaji na wala si kwa mikuki na bunduki.

Ni jukumu la wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanawajengea vijana matumaini ya Kenya iliyo bora zaidi, badala ya kuwatumbukiza vijana katika maafa yanayowaharibia mwanga wa matumaini na maendeleo. Vita na vurugu ni sera zilizopitwa na wakati kwani zinakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, kamwe vijana wasiruhusu kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya malengo yao binafsi!







All the contents on this site are copyrighted ©.