Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania afanya mazungumzo na Rais Francois Hollande wa Ufaransa
mjini Paris
Serikali ya Ufaransa imeipongeza Tanzania kwa uongozi wake katika kutafuta amani na
suluhu na majawabu ya migogoro mikubwa ya kisiasa Barani Afrika katika nchi za Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar, Zimbabwe na Somalia. Aidha, Ufaransa imeahidi
kuwa itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania na wananchi wake chini ya uongozi
imara wa nchi hiyo katika kujitafutia maendeleo. Msimamo huo wa Ufaransa umeelezwa,
Jumatatu, Januari 21, 2013, na Rais wa Ufaransa Mheshimiwa Francois Hollande wakati
alipomkaribisha kwenye Kasri ya Uongozi wa Ufaransa ya Elysee mgeni wake, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa mazungumzo.
Mazungumzo hayo yamehusu masuala ya uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa, masuala
ya kanda ya Afrika na kuhusu masuala ya kimataifa. Rais Kikwete ambaye yuko katika
ziara rasmi ya siku tatu ya Kiserikali katika Ufaransa kwa mwaliko wa Rais Hollande
amewasili kwenye Kasri ya Elysee kiasi cha saa tano asubuhi kamili baada ya kuwa amekaribishwa
rasmi kwa gwaride rasmi kwenye Jumba la Cour d’honneur des Invalides mjini Paris. Miongoni
mwa waliohudhuria sherehe hiyo ya kukaribishwa rasmi katika Ufaransa ni pamoja na
maofisa wa Serikali ya Ufaransa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika na nchi
nyingine katika Ufaransa pamoja na maofisa wanaofuatana na Rais Kikwete kwenye ziara
hiyo. Katika mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, Rais Hollande amemwagia sifa
Rais Kikwete na uongozi wa Tanzania kwa hatua na msimamo wao katika kutafuta suluhu
katika migogoro kwenye ukanda wa mashariki mwa Afrika katika nchi za DRC, Madagascar,
Zimbabwe na Somalia. “Tunaipongeza sana Tanzania na uongozi wako Mheshimiwa Rais
kwa jinsi mnavyohangaika kusaka amani na utulivu katika eneo la Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu (ICGLR)
katika nchi za DRC-Congo, Madagascar, Zimbabwe na kwa kiasi fulani katika Somalia,”
amesema Rais Hollande na kuongeza: “Pongezi hizi siyo za Ufaransa peke yake bali
ni pongezi zinazotolewa na viongozi na mataifa mengine duniani kwa sababu mnachofanya
kina manufaa ya dunia nzima.” Rais Hollande amesifia uhusiano mzuri ulioko kati ya
Tanzania na Ufaransa na kuahidi kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono jitihada za
Tanzania na Watanzania katika kujiletea maendeleo. Katika miaka mitano iliyopita,
Tanzania imenufaika na misaada ya Ufaransa katika maeneo mbali mbali likiwemo la sekta
ya maji kwa ajili ya miji midogo. Ufaransa imeipa Tanzania kiasi cha euro 50.9 kuchangia
maendeleo. Msaada huo ulianza kutolewa baada ya Rais Kikwete kufanya ziara ya Ufaransa
mwaka 2006 akiwa njiani kwenda Marekani. Katika kuongeza mchango wa ufaransa kwa kasi
ya maendeleo ya Tanzania, Rais Hollande ameyataka makampuni zaidi ya Ufaransa kuwekeza
katika uchumi wa Tanzania kuliko ilivyo sasa. Naye Rais Kikwete amemshukuru Rais
Hollande na Ufaransa kwa misaada ya maendeleo ambayo imekuwa inatolewa na nchi hiyo
katika miaka mingi ya uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili. Rais Kikwete pia amemshukuru
na kumpongeza Rais Hollande na Ufaransa kwa uamuzi wao “thabiti” wa kuunga mkono
wananchi wa Mali dhidi ya waasi wa nchi hiyo ambao walikuwa wanatishia kuiteka nchi
nzima ya Afrika Magharibi. “Hili la Mali siyo tatizo la Mali wala siyo tatizo la
Afrika. Hili ni tatizo la kibinadamu na binadamu ni wamoja bila kujadili wanaishi
katika eneo lipi la dunia yetu. Hivyo, tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi
wako thabiti kabisa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Tunapenda kutoa wito kwa
nchi nyingine duniani kujitokeza kuungana na Wafaransa katika kusaidia watu wa Mali,
kusaidia Ufaransa na kuisaidia Jumuiya ya ECOWAS katika kumaliza tatizo hilo la Mali.”
Ufaransa imeingiza majeshi yake katika Mali ili kuwarudisha nyuma waasi waliokuwa
wanaendelea na safari ya kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo wa Bamako. Mbali na kukutana
na Rais Hollande, Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Seneti,
Mheshimiwa Jean Pierre Bel; Kiongozi wa Mahedhebu ya Ismailia, H.H. The Aga Khan na
Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total (Upstream) Bwana Yves Louis Darricarrere.