2013-01-23 07:44:30

Katiba ya Tanzania: madaraka ya Rais, Tume huru ya Uchaguzi, Udini, Muungano, Haki ya kuishi na Umiliki wa Ardhi


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania mintarafu mwongozo wa uhamasishaji, leo katika makala haya wanazungumzia kuhusu madaraka ya rais, tume huru ya uchaguzi, dhana ya kuwa na Serikali isiyokuwa na dini, muungano na umiliki wa ardhi. RealAudioMP3
Madaraka ya Rais
Madaraka ya uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola - jaji mkuu na majaji na wabunge wa kuteuliwa. Vile vile huteua mkuu wa Jeshi la polisi, wakuu wa mikoa na wilaya nk. Pia ana mamlaka ya kusamehe wafungwa, kuvunja bunge na baraza la mawaziri nk. Madaraka haya yanaweza kutumiwa vibaya, na pia uwajibikaji kwa wateuliwa hao kwa wananchi unakuwa mdogo. Madaraka haya yapunguzwe na/ama yadhibitiwe. Vigezo viwe wazi na uamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.
Tume huru ya uchaguzi na Tume nyinginezo
Kwa sababu inaundwa kwa njia ya uteuzi bila vigezo kuwekwa wazi, wananchi wengi wamekosa imani nayo, na malalamiko yamekuwa mengi. Uundwaji wa Tume zetu ufanyike kwa uwazi na iliyo shirikishi.
Dhana ya kuwa Serikali haina dini (Secularity of the State)
Msingi huu ndio nguzo ya umoja na amani katika nchi yetu. Ifafanuliwe na kusimamiwa kikatiba ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka katika uhuru wa kuabudu kwa kuwa tumeshaona unatumika vibaya kama vile kuleta mgawanyiko na mtikisiko katika familia, kufanya mihadhara ya kukashifu dini nyingine, kuharibu mali za wengine na kusababisha uvunjifu wa amani. Vile vile msukumo wa kuanzisha mahakama ya kadhi ndani ya mfumo wa mahakama za nchi siyo haki kwa hiyo isiwemo katika Katiba kwa kuwa ni mambo ya kidini na huenda ni njia ya kuifikisha nchi yetu katika kukiuka dhana ya kuwa serikali yetu haina dini.
Muungano
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Katiba ya Muungano imevunjwa, wakati huo huo msukumo wa watu kutaka Muungano uangaliwe upya una hoja zenye nguvu. Tutoe maoni yetu tukizingatia sababu za waasisi wa muungano, na pia faida na hasara za muungano kwa wakati huu. Mapendekezo ya kutambua Tanganyika kama nchi yametambuliwa na Katiba ya sasa ya Zanzibar, kwa hiyo wazo la kuwa na Muungano wenye Serikali tatu ni hoja ambayo tunaweza kutolea maoni yetu.
Haki ya kuishi
Kwetu sisi Wakatoliki ni jambo la kupigania kwa nguvu zote Katiba iweze kulinda uhai tangu kutungwa mimba. Vile vile tunaweza kutoa maoni yetu juu ya adhabu ya kifo. Hapa tuna wajibu wa pekee kabisa kutoka imani yetu inayotufundisha kwamba mwenye mamlaka ya kutoa uhai na kuutwaa ni Mungu Mwenyewe.
Umiliki ardhi
Haki ya watu wa Tanzania Visiwani kumiliki ardhi ya Bara ifutwe kama ilivyo kwa watu kutoka Tanzania Bara kutoweza kumiliki ardhi huko Visiwani.








All the contents on this site are copyrighted ©.