Ukeketaji ni mila na desturi zilizopitwa na wakati
DR. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, hivi karibuni
alisema kwamba, anaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupiga rufuku mila
na desturi zilizopitwa na wakati, zinazoendelea kuleta madhara na usumbufu mkubwa
miongoni mwa wanawake, kiasi cha kuwanyima haki zao msingi. Mila za ukeketaji bado
ziko katika Jamii nyingi za Kiafrika na sehemu nyingine za dunia.
Dr. Tveit
anasema, kama kiongozi wa Kanisa anaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja
na wanaharakati mbali mbali, ambao wameendelea kusimama kidete kulinda na kutetea
haki msingi za wanawake, dhidi ya mila na tamaduni zilizopitwa na wakati, zinazoendeleza
nyanyaso kwa wanawake na wasichana sehemu mbali mbali za dunia.
Ukeketaji
una madhara makubwa kwa maisha ya wasichana na wanawake, wakati mwingine, mila hizi
zimepelekea vifo vya wanawake na wasichana kutokana na kutokwa na damu kwa wingi.
Ni mila ambayo imewasababishia wanawake kupata maumivu makali wakati wa kujifungua
na hivyo kuhatarisha maisha yao wenyewe na watoto wanaowabeba tumbaoni mwao.
Anaunga
mkono juhudi za kutokomeza mila na desturi zilizopitwa na wakati, kwani wanawake wanapaswa
pia kuheshimiwa na kuthaminiwa utu na heshima yao! Dr. Tveit ameyasema hayo hivi karibuni
alipokuwa anashirikisha mawazo yake na Wanaharakati wa kimataifa wanaopinga mila na
desturi zilizopitwa na wakati dhidi ya utu na heshima ya wanawake, alipokutana nao
kwenye Makao Makuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni.
Anasema, Baraza la Makanisa
Ulimwenguni, Mwezi Oktoba 2013, litafanya Mkutano Mkuu, huko Busan nchini Korea. Mada
itakayoongoza Mkutano huu ni "Mungu wa uhai, tuongoze katika haki na amani".Anasema,
imani yao kwa Mungu wa uhai ndiyo inayowawajibisha kusimama kidete kupinga mila na
desturi zinazomdhalilisha mwanamke. Kuna idadi kubwa ya wasichana ambao maisha yao
yako hatarini kutokana na baadhi ya Jamii kuendekeza mila na desturi za ukeketaji,
ambazo kwa sasa zimepitwa na wakati.
Dr. Tveit anaungana na viongozi mbali
mbali wa kidini kupinga vitendo vya unyanyasi wa kijinsia wanavyofanyiwa wanawake
kwa kisingizio cha kuendeleza mila na desturi, hata kama zimepitwa na wakati. Haki
msingi za wanawake zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa.