Siku ya tano ya kuombea Umoja wa Wakristo: kutembea kama rafiki wa Yesu
Katika siku hii ya tano wazo letu kuu ni Kutembea kama rafiki wa Yesu. Kutembea kinyenyekevu
na Mungu hakumaanishi kutembea pekee kama nafsi moja - ina maana kutembea na wale
ambao ni ishara za uwepo wa Mungu kati yetu, marafiki zetu. “Nimewaita ninyi rafiki"
anasema Yesu katika Injili ya Yohane. Katika uhuru
wa upendo tunaweza kuchagua marafiki zetu na kuchaguliwa kuwa marafiki. “Hamkunichagua
mimi bali ni mimi niliyewachagua ninyi”, Yesu anatufundisha. Urafiki na Yesu unapita
fikara na mahusiano yetu ya kifamilia na kijamii. Inahusiana na upendo wa kudumu wa
Mungu kwa viumbe vyote. Wimbo wa Mfalme Sulemani umetafsiriwa kwa namna mbalimbali
kama wimbo wa upendo wa Mungu kwa waisraeli, au upendo wa Kristu kwa kanisa. Ile hamu
waliyonayo wanaopendana ndio ushuhuda wa pekee unaopita mipaka ya kijamii. Upendo
wa Mungu unawafikia kwa karibu sana wenye dhiki. Watu wenye dhiki wanajua kuwa wakati
Mungu anawaangalia anafanya hivyo katika upendo wake. Yesu anawaambia watu wenye
dhiki kuwa “nimewaita ninyi rafiki”. Ni aina ya kukombolewa kutoka katika utumwa wa
manyanyaso na dharau inayoletwa na matabaka ndani ya jamii. Watu wenye dhiki hivyo
wana wajibu wa kuwa marafiki wa Yesu. Na Mungu anatutaka tufanye nini sisi ambao tunaitwa
kutembea naye kama marafiki zake? Kanisa linaitwa kuwakumbatia wenye shida popote
lilipo kama marafiki wa kawaida. Wito huu wa kuwa marafiki na marafiki wa Yesu
ni namna nyingine ya kuelewa umoja wa kanisa ambao tunaomba wiki hili. Wakristo kutoka
kona zote za dunia wanaitwa kuwa marafiki na wale wote wanaopambana na ubaguzi na
madhulumu. Kutembea katika umoja wa Kanisa kunatuhitaji kutembea kinyenyekevu na Mungu
na kama marafiki wa Yesu. SALA Ee Yesu toka mwanzo wa uhai wetu umejitoa kwetu
kama rafiki yetu. Upendo wako unawakumbatia wanadamu wote, hasa wale waliotengwa na
kukataliwa kwa sababu ya tofauti za madaraja, utaifa, rangi, walizojitengenezea watu.
Tukiwa tumejawa na uthabiti na uhakika wa heshima tuliyo nayo kwako, tunaweza kutembea
pamoja kwa umoja kumwendea kila mmoja wetu na kumpokea na kumkumbatia katika roho,
kama mwana wa Mungu. Mungu wa uzima tuongoze katika njia ya haki na amani. Amin. MASWALI Je,
ni watu gani walioko katika jumuia yako ambao Yesu anakuita kujenga urafiki nao? Ni
kitu gani kinawazuia marafiki wa Yesu yaani sisi, kuwa marafiki sisi kwa sisi? Je,
ni kwa jinsi gani kuwa marafiki wa Yesu mwenyewe kunalipa changamoto Kanisa lililogawanyika? Tafakari
hii imeandaliwa na Padre Emmanuel Nyaumba.