Maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania: uteuzi wa viongozi, huduma bora za kijamii, haki
za binadamu, ukubwa Serikali na Bunge; mgawanyo wa madaraka
Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba hivi karibuni
amenukuliwa akisema kwamba, Mwezi Februari, 2013, Tume itaanza kuchambua maoni na
baadaye, kuandika Rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania inayotarajiwa kuwa imekamilika
mwezi Juni, 2013. Hatua itakayofuatwa ni kupelekwa kwa Mabaraza ya Kikatiba na kwamba,
Tanzania inatarajia kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015. Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania linaendelea kuhamasisha waamini na watanzania wenye mapenzi mema
kuangalia changamoto zifuatazo ili ziweze kufanyiwa kazi wakati wa kuandika Katiba
Mpya: Uteuzi wa viongozi; huduma bora za kijamii na haki za binadamu; ukubwa wa Serikali
na Bunge; Mgawanyo wa madaraka pamoja na Madaraka ya Rais.
Kwa mujibu wa Katiba
ya sasa Rais ana madaraka makubwa mno. Vigezo vinavyotumika haviko wazi na mara kadhaa
imeonekana wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu wamepewa kazi ambayo hawana
uwezo nayo. Hata inapodhihirika hivyo bado imekuwa vigumu mno kuwaondoa madarakani.
Vigezo vya kidini na kinasaba pia vimekuwa vikilalamikiwa kuwa vinatumika.
Kwa mteuliwa husukumwa kutumikia matakwa ya aliyemteua badala ya kuwa mtumishi wa
wananchi. Katiba ijibu changamoto hii kwa kuweka sifa na vigezo kadiri ya mahitaji
ya nafasi husika na pia njia ya kuwajibisha. Uteuzi usibaki kwa mtu mmoja bali ufanyike
kwa njia shirikishi kupitia Tume huru.
Huduma bora za jamii na haki za binadamu
Haki
hizi ni pamoja na huduma za afya, elimu, maji, miundombinu nk. Haki hizi zaweza kulenga
mtu mmoja mmoja , makundi maalum kama vile walemavu, wazee na maskini ama jamii
nzima. Kutimiza haki hizi serikali na wananchi wote wanawajibika kila mmoja kwa nafasi
na kiwango chake. Haki hizi ziainishwe katika Katiba na Katiba ihakikishe zinatekelezeka
kisheria.
Ukubwa wa Serikali
Tunaweza kuwa na serikali ndogo ambayo
inafanya kazi kwa ufanisi. Hapa tuangalie idadi ya wizara na mawaziri, na hata mgawanyo
wa mikoa na wilaya. Tunaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupunguza maeneo
haya na hivyo kuweza kuongeza fungu katika bajeti ya maendeleo na mahitaji mengine
muhimu ambayo tunakwama kuyagharamia. Katiba iainishe hayo isiwe ni matakwa ya kila
awamu ya uongozi.
Ukubwa wa Bunge
Kwa nia hiyo hiyo ya kupunguza gharama
inafaa kuangalia upya nafasi za ubunge wa kuteuliwa na wa viti maalum. Kimsingi mbunge
ni mwakilishi wa wananchi ambao wanaweza kumwajibisha, na aelewe anabeba dhamana kubwa
na anapaswa kuchapa kazi kwa umahiri na weledi.
Mgawanyo wa madaraka
Hii
ni kanuni msingi ya demokrasia na utawala bora. Kibinadamu ni jambo msingi kwa sababu
inatoa nafasi ya kusahihishana na hivyo kukabiliana na madhaifu ya kimaumbile. Mihimili
mikuu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali yapasa vifanye kazi kwa uwajibikaji na
kuwajibishana na sio katika mwingiliano. Kwa hali ilivyo sasa tunaona kuna mwingiliano
mkubwa na hata tunaona serikali hukimbilia mahakama (isiyo huru) kama kichaka kuficha
udhaifu katika utendaji wa majukumu yake, hasa kukwepa kutimiza haki za watu.
Kwa
namna hii utawala wa sheria unakuwa mgumu kudhihirika. Katiba iimarishe kanuni hii
kwa kutoruhusu wabunge kuwa mawaziri, majaji kutoteuliwa na Rais nk. Wananchi wapewe
uwezo wa kudhibiti mihimili ya dola kwa kuweka Mahakama ya Katiba kupeleka mashauri
yao pale wanapoona kuna ukiukwaji wa Katiba katika utekelezaji wa majukumu yao.
Madaraka
ya Rais
Madaraka ya uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia
mihimili mingine ya dola - jaji mkuu na majaji na wabunge wa kuteuliwa. Vile vile
huteua Mkuu wa Jeshi la Polisi, Wakuu wa mikoa na wilaya nk. Pia ana mamlaka ya kusamehe
wafungwa, kuvunja Bunge na Baraza la Mawaziri nk. Madaraka haya yanaweza kutumiwa
vibaya, na pia uwajibikaji kwa wateuliwa hao kwa wananchi unakuwa mdogo.
Madaraka
haya yapunguzwe na/ama yadhibitiwe. Vigezo viwe wazi na uamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.