Rais Obama aapa kuongoza Marekani kwa kipindi kingine cha miaka 4
Rais Barack Obama wa Marekani, Jumapili, tarehe 20 Januari 2013 aliapishwa rasmi kuanza
awamu ya pili ya uongozi wake kwa miaka mingine minne. Ameapa kulinda na kutetea katiba
ya nchi. Hafla hii imehudhuriwa na watu wachache kwani ilikuwa ni utekelezaji wa Katiba
inayosema kwamba, Rais baada ya kuchaguliwa atapaswa kuapishwa tarehe 20 Januari.
Wakati
huo huo, Makamu wa Rais Joe Biden aliapishwa mapema asubuhi na baadaye kwa pamoja
walikwenda kutoa heshima na kuweka shada la maua kwa Askari wa Marekani waliopoteza
maisha vitani. Awamu ya Pili ya uongozi wa Rais Obama unakabiliwa na changamoto ya
kuendelea kufufua na kurekebisha uchumi; kuweka bayana sera kuhusu wahamiaji pamoja
na mkakati wa kudhibiti silaha za moto nchini Marekani.
Utamaduni wa kuachiana
madaraka kwa njia ya amani ni tukio ambalo linawaunganisha Wamarekani wote kwa kuweka
kando misimamo yao ya kisiasa, ili kuonesha umoja wa kitaifa na ukomavu wa kisiasa
na kidemokrasia.