2013-01-19 10:03:38

Waamini jengeni utamaduni wa upatanisho ili kukuza na kuimarisha haki na amani!


Askofu mkuu Augustine Kasujja, Balozi wa Vatican nchini Nigeria anawaalika Wakristo nchini humo kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha licha ya madhulumu wanayoendelea kukabiliana nayo na kwamba, vitendo hivi visiwakatishe tamaa, bali waendele kusimama kidete katika imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Askofu Kasujja anasema kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, Wakristo nchini Nigeria wamekabiliwa na changamoto kubwa, kiasi hata cha kutikiswa katika misingi ya imani yao kutokana na madhulumu ya kidini yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali nchini Nigeria.

Wakristo watambue kwamba, ushindi unapatikana kwa njia ya kukumbatia Msalaba, kama alivyofanya Kristo mwenyewe katika Fumbo la Pasaka. Kama wafuasi wa Kristo wanatumwa na kuchangamotishwa kuendelea kuwa ni wajenzi wa misingi ya haki, amani, mshikamano na upatanisho wa kitaifa. Ufalme wa Kristo uko imara na thabiti, kwani Falme za dunia zitakuja na kutoweka kama ndoto ya mchana, kama zilivyokuwa tawala mbali mbali za kidunia, jambo la msingi ni Wakristo kuendelea kutolea ushuhuda imani, matumaini na mapendo.

Askofu mkuu Augustine Kasujja anasema, Nigeria inahitaji kujenga utamaduni wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa, ili kutoa fursa kwa watu wa dini na madhehebu mbali mbali kuweza kuishi kwa amani, upendo na mshikamano bila kubaguana kwa misingi ya kidini, kikabila na mahali anapotoka mtu!







All the contents on this site are copyrighted ©.