Mikakati ya kichungaji kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
na mbinu mkakati wa kupata suluhu ya vita nchini DRC ni kati ya mambo yaliyojadiliwa
na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, lililohitimisha mkutano
wake wa Mwaka hivi karibuni, huko Muyinga, nchini Burundi.
Maaskofu wanasema
kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni kipindi cha neema na baraka na changamoto
kwa waamini kuchuchumilia wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, sanjari na kuhakikisha
kwamba, Kanisa linaendelea kuhamasisha ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu
hasa katika nchi zile ambazo bado kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Maaskofu
wameibua Mkakati wa pamoja wa shughuli za kichungaji kwa kufanya hija za mshikamano
kwa wakimbizi kutoka DRC wanaoishi kwenye Kambi za Wakimbizi nchini Burundi na Tanzania.
Maaskofu wanapenda kukuza na kudumisha elimu ya haki na amani katika nchi zao kwa
kuendelea kujikita katika dhamana ya upatanisho, changamoto kutoka kwa Mababa wa Awamu
ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika ya Kati wanataka kuunganisha mikakati yao pamoja na Shirikisho la
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika mchakato wa
ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho.
Maaskofu wanaialika Familia
ya Mungu Barani Afrika, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu;
kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu pamoja na kuendelea kuwa
ni wajenzi wa amani katika nchi zao, kwa kukataa katu katu sera za chuki, uhasama
na ubaguzi, badala yake, kujenga na kuimarisha haki, amani, upendo na mshikamano wa
kweli.