2013-01-18 09:53:46

Kongamano la Kimataifa kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi Afrika ya Kusini, Miaka 30 tangu ulipogunduliwa duniani!


Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili katika Waraka wake wa Kichungaji, Kanisa Barani Afrika anabainisha kwamba, licha ya umaskini wa kutopea, ujinga na maradhi, lakini, Ukimwi umekuwa ni janga kubwa kwa nchi nyingi Barani Afrika, changamoto ya kuwa waaminifu katika maisha ya ndoa, kujizuia pamoja na kudumisha misingi ya maadili na utu wema. Ukimwi ni changamoto kwa wote kwani hauchagui wala haubagui kwani madhara yake pia ni makubwa katika maendeleo ya watu kijamii, kiuchumi na kiroho.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika waraka wa kichungaji, Dhamana ya Afrika anabainisha kwamba, Ukimwi ni changamoto ya kitabibu na kimaadili; kwani kinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi lazima ijikite katika malezi ya kijinsia yanayobubujika katika sheria asilia, yakiangaziwa na kweli za Kiinjili na Mafundisho ya Kanisa. Juhudi zote hizi zinalenga kwa namna ya pekee kutetea zawadi ya uhai.

Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikishi la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, akichambua kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi mintarafu changamoto zilizotolewa na Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika anabainisha kwamba, hii ni changamoto ya kubadili tabia na kwamba, ni sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu wa binadamu sanjari na juhudi za kudumisha haki, Kanisa linapaswa kushirikisha mchango wake makini katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, kwa kuonesha upendo na mshikamano na wote walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi.

Ni katika mwelekeo huu kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, kuanzia tarehe 20 hadi 22 Januari 2013, litafanya Kongamano la Kimataifa, ili kupembua mchango wa Kanisa Katoliki katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi, Afrika ya Kusini, miaka thelathini tangu ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza duniani. Kanisa linaangalia juhudi hizi mijini na vijijini, changamoto ya kutubu na kuongoka; kuendeleza mshikamano wa huduma na madhehebu pamoja na dini mbali mbali. Maadili, utu na heshima ya mwanadamu ikipewa kipaumbele cha kwanza.

Wajumbe wa Kongamano hili kutoka sehemu mbali mbali Barani Afrika, wanatarajia kupembua kwa kina Ukimwi na maisha ya vijana; maongozi ya maisha ya kiroho, huduma kwa waathirika wa Ukimwi. Kuna mada itakayozungumzia upimaji wa Ukimwi kwa Majandokasisi wanaotaka kuwa Mapadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.