2013-01-18 07:34:40

Juma la kuombea Umoja wa Wakristo: mshikamano na wote wanaodhulumiwa kutokana na Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!


Makanisa yanapoadhimisha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania limeandika barua ya kichungaji, kama kielelezo cha mshikamano na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoendelea kukumbana na madhulumu kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa bahati mbaya, madhulumu haya yanaendelea kujionesha katika nchi kama vile Pakistani, Nigeria, Misri na Sudan. RealAudioMP3
Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali, ili madhulumu haya yaweze kukoma na watu kuishi kwa amani na utulivu, huku wakiheshimiana na kuthaminiana kama watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Madhulumu ya kidini ni jambo ambalo ni kinyume kabisa cha uhuru wa kidini ambao ni nguzo thabiti ya haki zote msingi za binadamu.
Maaskofu Katoliki Hispania wanakumbusha kwamba, Sala na Tafakari kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo zimeandaliwa na Wakristo kutoka India, kwa kuwahusisha watu wanaoendelea kubaguliwa kutokana na matabaka ya kijamii nchini India. Kumbe, kuna haja ya kusali ili kuombea Umoja wa Wakristo sanjari na kuonesha mshikamano wa dhati na wote wanaoendelea kudhulumiwa kutokana na Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili haki na uhuru wa kuabudu uweze kuheshimiwa na wote.
Kanisa halina budi kusonga mbele katika mchakato wa kuhamasisha haki, amani na mshikamano, likijitahidi pia kuponya madonda ya kurasa chungu zilizopita katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kuombea umoja wa Kanisa katika maisha ya kiroho, yanayopata chimbuko lake katika Sala endelevu pasi na kuchoka wala kukata tamaa; toba na wongofu wa ndani; kwa kukiri makosa yaliyojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuanza hija ya upatanisho wa Kiekumene.
Kanisa halina budi kuendeleza Majadiliano ya upendo katika mchakato wa kiekumene, yanayojidhihirisha wazi katika huduma zinazotolewa na Makanisa sehemu mbali mbali za dunia katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Kanisa linapaswa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; ut una heshima yak ila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; pamoja na kutetea misingi ya amani, utulivu na mshikamano. Ndoa na Familia, vipewe nafasi yake katika vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa. .
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linakumbusha kwamba, hivi karibuni, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Mwezi Oktoba, 2013, litafanya mkutano wake mkuu wa kumi, unaoongozwa na kauli mbiu “Mungu wa maisha, tuongoze katika haki na amani”. Wakristo wanakusanyika kwa ajili ya kuombea Umoja, wakati huu, Kanisa Katoliki linapoadhimsiha Mwaka wa Imani, sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican; mtaguso ambao ulijikita kwa namna ya pekee katika kuonesha dira na mwongozo wa kwa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kwa kukazia: Majadiliano ya kiekuemene na kidini; Utume wa Kanisa katika Ulimwengu mamboleo; Utu na heshima ya mwanadamu.
Maaskofu Katoliki Hispania wanaangalia pia madhara makubwa yaliyojitokeza kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa; changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kubadili mtindo wa maisha, kwa kuwa na kiasi na kwamba, mikakati na sera za uchumi na maendeleo endelevu, zitoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Lengo ni kuwa na uhusiano mzuri kati ya uzalishaji, ugavi na ulaji.







All the contents on this site are copyrighted ©.