2013-01-17 15:20:21

Zingatieni sheria za maabara na jikiteni katika maboresho ya huduma za afya!


Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii Dr. Hussein Mwinyi ameitaka bodi ya maabara binafsi za afya kuchukua hatua kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria ikiwepo kusimamisha huduma na kuwapeleka mahakamani wale watakaokaidi sheria ya kuratibu huduma za maabara binafsi za afya. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Alhamisi tarehe 17 Januari 2013 alipokuwa akizindua bodi mpya ya maabara binafsi za afya .Alisema sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza kutumika mwaka 1998 ilikuwa na lengo la kuboresha huduma za maabara pamoja na kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya nchini.
“Uboreshaji wa mabadiliko ya sekta ya afya ni vema ufanyike sambamba na uboreshaji wa huduma za maabara ikiwemo uzingatiwaji wa maadili ya utoaji wa huduma za maabara ili kuepuka athari zinazoweza kutokea kwa mtoa huduma au anayehudumiwa yaani mgonjwa”alisema Aidha, aliitaka bodi hiyo kuratibu na kukagua majengo,vifaa,vitendanishi na kuhakikisha usahihi wa majibu ya vipimo ili kuleta ubora wa matokeo ya uchunguzi wa magonjwa pamoja na kutoa nafasi kwa wataalamu wa maabara kuanzisha huduma hiyo hapa nchini.
“Kazi ya bodi hii ni ya muhimu sana kwani utoaji wa huduma ya tiba haukamiliki iwapo hakuna huduma ya uchunguzi wa magonjwa,ikiwemo maabara,hivyo maabara inapofanya kazi zake kwa usahii,inampa nafasi nzuri mganga kuwa na usahii wa tatizo la mgonjwa na kutoa dawa inayostahili na kutuonesha umuhimu wa kuwa na wataalamu wazuri wa maabara”. Hata hivyo Waziri huyo ameitaka bodi hiyo kupitia na kufanya maboresho mapya ya sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili iandane na mabadiliko yanayojitokeza na kuweza kusimamia na kusajili maabara zote nchini.
Awali akisoma hotuba yake Mwenyekiti wa bodi hiyo Dr. Magraret Mhando alisema bodi yake inatarajia kuhakikisha kuwa vifaa na vitendanishi vyote vinavyotumika nchini vina ubora unaokubalika na vimeorodheshwa katika orodha ya vifaa na vitendanishi vya maabara ya afya pamoja na kusajili na kuandikishwa maabara na maduka yote kwa mujibu wa sheria.
Bodi mpya ya maabara binafsi za afya inaundwa na wajumbe wapatao kumi inatarajia kumaliza muda wa utendaji wake kwa miaka mitatu mwaka 2015.








All the contents on this site are copyrighted ©.