2013-01-17 14:54:34

Wakristo tembeeni katika unyenyekevu unaoonesha haki, huruma na unyofu wa moyo, kwa kukumbatia ukweli, ili muwe ni nguzo ya furaha na matumaini kwa wengi!


Kile ambacho Bwana anataka kutoka kwetu ni kutenda haki, kupenda rehema na kutembea katika fadhila ya unyenyekevu. Kipindi cha Noeli, kilichohitimishwa kwa Sherehe za Ubatizo wa Bwana, kimeonesha hija ambayo Mwenyezi Mungu amefanya pamoja na binadamu na katika utimilifu wa nyakati, Neno wa Mungu akafanyika mwili, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumwongoza katika hija ya utakatifu, haki na amani.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa Ujumbe wa Kiekumene kutoka Finland, uliomtembelea mjini Vatican, siku ya Alhamisi, tarehe 17 januari 2013 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Henrik, msimamizi wa nchi ya Finland. Baba Mtakatifu anasema, kutembea kwa unyenyekevu mbele ya Bwana ni kuonesha utii pamoja na kutekeleza ujumbe wake ambao ameudhihirisha katika Mpango wake, kama kielelezo cha imani na hija ya kiekumene, kwa kujikita katika mchakato unaopania kupata umoja kamili miongoni mwa Wakristo.

Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia njia ya uaminifu kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu bila kukatishwa tamaa kutokana na magumu na vikwazo vinavyoweza kujitokeza. Ili kufanikisha jukumu hili, wakristo katika ujumla wao wanapaswa kujikita katika maisha ya Sala; kuchuchumilia utakatifu sanjari na kufanya tafiti za kina kuhusiana na masuala ya kitaalimungu; umoja na mshikamano katika huduma kwa Mungu na jirani, ili kujenga dunia inayosimikwa katika haki na upendo.

Katika Tamko la pamoja lililotolewa kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri linaonesha kwamba, Wakristo kwa pamoja wamekubaliwa na wamempokea Roho Mtakatifu anayeendelea kuwapatia upya wa maisha na kuwaalika kutenda kazi njema.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwamba, hija ya kiroho ya wajumbe wa Kiekumene kutoka Finland, itaendelea kuimarisha mshikamano wa kiekumene miongoni mwa Wakristo nchini humo. Anamshukuru Mungu kwa mafanikio mbali mbali yaliyokwishafikiwa hadi sasa pamoja na kuendelea kumwomba Roho Mtakatifu awaongoze Wakristo katika upendo na umoja, daima wakijitahidi kuishi katika mwanga wa Injili ili kutoa mwanga mkubwa zaidi katika kukabiliana na changamoto za kimaadili zinazoendelea kujitokeza katika Jamii.

Wakristo wanapojitahidi kutembea katika fadhila ya unyenyekevu inayojionesha katika haki, huruma na unyofu wa moyo; wataweza kukumbatia ukweli na kuwa nguzo za furaha na matumaini kwa wote wanaotafuta kigezo makini cha rejea katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi ya ajabu. Amewahakikishia uwepo wake wa karibu na sala katika Mwanzo wa Mwaka Mpya wa 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.