2013-01-17 08:12:37

Uhusiano kati ya Vatican na Serikali ya Italia


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeanza hija ya kitume mjini Vatican, inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano, ili kutoa taarifa ya maisha, utume na mikakati ya majimbo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Mabaraza ya Kipapa. RealAudioMP3

Maaskofu wa Italia wanafanya hija hii wakati ambapo Italia inakabiliwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa, kijamii, kimaadili na kiutu. Takwimu zinaonesha kwamba, Italia imeendelea kukabiliwa na hali ngumu ya uchumi kuanzia mwaka 2009 hadi wakati huu.

Hii ni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, zilizopelekea ukuaji wa uchumi wa Italia kudorora kwa kiasi kikubwa na hivyo deni la taifa kuongezeka kwa asilimia 120%. Tatizo la ajira nchini Italia, kwa sasa ni asilimia 11%, lakini waathirika wakubwa ni vijana. Kutokana na kushuka kwa soko la ndani na nje, makampuni na viwanda vingi vimejikuta vikilazimika kufunga shughuli zake za uzalishaji au kuhamia katika nchi nyingine, wakiwa na tumaini la kupata walau faidia kidogo kutokana na kupanda mno kwa gharama za uzalishaji nchini Italia na Jumuiya ya Ulaya katika ujumla wake.

Waziri mkuu Mario Monti na Serikali yake ya kipindi cha mpito, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ililazimika kubuni mbinu mkakati wa kupunguza matumizi, kuongeza pato, kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kurudisha imani kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya Italia. Huu ni mkakati ambao umewalazimisha wananchi wengi wa Italia kujifunga kibwebwe ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha, kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha wakati huo hali ya maisha ikishuka kwa kasi kubwa, kutokana na watu wengi kukabiliwa na hali ya umaskini wa kipato kutokana na ukosefu wa fursa za ajira. Hali ya umaskini ni mbaya zaidi kwa familia zenye watoto zaidi ya mmoja.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 11 Februari 1929, Serikali ya Italia, chini ya uongozi wa Benito Mussolini na Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican, pande hizi mbili ziliwekeana Mkataba unaojulikana kuwa ni Mkataba wa Laterano, ambao ulitoa uhuru kamili wa Vatican kuwa ni nchi inayojitegemea katika mambo yake. Serikali ya Italia, ikakubaliana na kushirikiana na Kanisa katika masuala ya kidini, sheria za ndoa pamoja na sekta ya elimu.

Kunako tarehe 18 Februari 1984, Waziri mkuu wa wakati huo, Bertino Craxi kwa niaba ya Serikali ya Italia na Kardinali Agostino Casaroli kwa niaba ya Vatican walifanya marekebisho makubwa katika Mkataba wa Laterano. Dini ya Kikatoliki iliyokuwa inatambuliwa kuwa ni dini ya Serikali na Nchi ya Italia kwa ujumla, ikaondolewa katika Katiba ya Nchi, ili kutoa uhuru wa kidini kwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Italia.

Uteuzi wa Maaskofu wa Italia, ukawa unafanywa moja kwa moja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, bila kuhitaji kwanza kibali kutoka Serikali ya Italia. Kuhusiana na masuala ya fedha na uchumi, waamini na wananchi wenye mapenzi mema, wakapewa uhuru wa kuchangia katika utume wa Kanisa kadiri ya sheria za nchi. Utekelezaji wa mpango mkakati huu ukaanza kunako mwaka 1987. Na fedha inayotolewa na waamini pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa inadhibitiwa kikamilifu na Kanisa pamoja na Sheria za Nchi.

Hii ndiyo fedha ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, limekuwa likitumia kwa ajili ya kusaidia kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo katika Makanisa ya Kimissionari sehemu mbali mbali za dunia na msaada wa dharura kwa watu wanaokumbwa na majanga asilia. Baraza la Maaskofu Katoliki linawajibika kutoa taarifa ya fedha zilizokusanywa na matumizi yake. Sheria hii pia inayahusu Madhehebu mengine ya Kikristo yanayotekeleza utume wake nchini Italia.

Utafiti na upembuzi wa kina uliofanywa kuhusiana na tunu msingi hususan: maisha, familia, kazi, dini, siasa na jamii zinabainisha kwamba, wananchi wengi wa Italia bado wana mwamko wa imani kwa Kanisa Katoliki, ikilinganishwa na nchi nyingine 48 kutoka Ulaya.

Bado kuna waamini wanaoshiriki kikamilifu katika Ibada zinazofanyika kila juma, ingawa pia kuna asilimia ishirini ya watu ambao kwa sasa wameshindwa kuona tena mlango wa Kanisa. Tatizo kubwa linalojitokeza kwa sasa ni kuhusiana na kweli za Kiimani, uhusiano na taasisi za kidini na kile mwamini anacho amini kutoka katika undani wa maisha yake.

Kwa ufupi, hii ndiyo hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Italia, wakati huu Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linapoendelea na hija yake ya kitume mjini Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.