Kanisa liko huru kutekeleza wajibu wake na wala halifungwi na Serikali wala Mfumo
wowote wa Kisiasa
Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na Ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican anasema Kanisa liko mstari wa mbele kulinda na kutetea
uhuru wa kidini na dhamiri nyofu mintarafu maadili, chapa ya mtu katika masuala ya
kidini, utu na heshima ya binadamu, kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita, hivi karibuni alipokuwa anazungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi
wa nchi na mashirika ya kimataifa mjini Vatican.
Hizi ni nguzo msingi zinazopania
kudumisha uhuru na demokrasia. Kuna masuala tete kama vile utoaji mimba na ndoa za
watu wa jinsia moja ni mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Askofu
mkuu Mamberti anafafanua masuala haya kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Ulaya uliotolewa
kuhusiana na mfanyakazi mmoja kutoka Uingereza aliyekatazwa kuvaa Msalaba sehemu ya
kazi. Pili ni kesi ya mtumishi mmoja aliyekuwa anapingana na Mafundisho na Sheria
za Kanisa, kutaka kuendelea kuajiriwa.
Katika Mafundisho Tanzu, Kanisa linafafanua
kwamba, liko huru na linatekeleza dhamana na utume wake kwa kuzingatia mafao ya wengi
na kuheshimu sheria ambazo zinasimamia haki na wala halifungwi na mfumo wowote ule
wa kisiasa. Linaheshimu na kuthamini uhuru wa kidini pamoja na Sheria za Kimataifa.
Kanisa limejikuta kwa nyakati tofauti, likitakiwa kusimama kidete ili kutetea
msimamo na uhuru wake dhidi ya Serikali na Mifumo ya Siasa, iliyotaka kuupokonya uhuru
wa Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, utamaduni wa nchi nyingi za Ulaya, unataka kukumbatia
mawazo mepesi mepesi, ulaji wa kupindukia na ubinafsi, kiasi cha kushindwa kuheshimu
asili ya Kanisa ambalo ni Jumuiya ya Waamini inayoongozwa kwa misingi ya imani na
akili.
Katika mazingira kama haya anasema Askofu mkuu Mamberti inakuwa ni vigumu
kubainisha uhusiano kati ya viongozi wa Serikali na Jumuiya mbali mbali za kidini
katika Jamii yenye mchanganyiko mkubwa wa watu mintarafu mshikamano wa kijamii na
mafao ya wengi. Katika mazingira kama haya, Vatican inakazia umuhimu wa kuheshimu
uhuru wa kidini katika ujumla wake pamoja na kuzingatia mwelekeo wa kijamii, unaoheshimu
mtu binafsi na masuala ya kidini katika ujumla wake.
Kanisa linataka sheria,
kanuni na taratibu za Jamii ziweze kuheshimiwa, lakini pia Jumuiya za kidini ziwe
ni mahali ambapo uhuru wa kidini, amani na utulivu vinazingatiwa. Mafundisho haya
yanapata chimbuko lake katika uhuru na yanaweza kutumika kwa dini zote bila ubaguzi.