2013-01-16 08:57:37

Kwa miaka 10 mfululizo Idara ya Uchapaji ya Vatican imeendelea kujipatia faida!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 15 Januari 2013 amebariki na kufungua ofisi mpya za idara la uchapaji ya Vatican (LEV) na kusema kwamba, uwekezaji katika majengo wakati huu wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni kutaka kufanya maboresho makubwa zaidi kwa Idara ya uchapaji ambayo ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni mwendelezo wa dhamana na utume wa Mama Kanisa katika Uinjilishaji Mpya kwa kusoma alama za nyakati na kutumia kikamilifu kila fursa inayopatikana kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Bertone, anaupongeza uongozi pamoja na wafanyakazi wa Idara ya Uchapaji ya Vatican kutokana na umakini, weledi na majitoleo yao ambayo yameiwezesha Idara hii kuendelea kupata faida kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo. Ni Idara ambayo iko mstari wa mbele katika kuchapisha Mafundisho ya Kanisa, Liturujia na inaendelea pia kuchangia ustawi na maendeleo ya utamaduni wa Kikatoliki ndani na nje ya Italia.

Kwa kuwa na ofisi mpya, wafanyakazi katika Idara hii wanachangamotishwa kujipanga vyema zaidi, kwa kujiwekea malengo ya muda mrefu na mfupi; wakipania kutoa huduma bora zaidi kwa kuingia pia katika matumizi ya uchapaji wa vitabu kwa njia ya mtandao.

Kardinali Tarcisio Bertone anaungana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuwatia moyo ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini ya kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa zaidi, wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.