2013-01-16 14:56:27

Juma la kuombea Umoja wa Wakristo: Kile ambacho Bwana anataka kutoka kwetu!


Kipindi cha Noeli, Mama Kanisa alipata bahati ya kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, linalotanabainisha Ufunuo wa Mungu kwa Waisraeli, uliojionesha kwa namna ya pekee kwa Musa na Manabii wa Mungu walioendelea kuweka hai matumaini ya Waisraeli katika utekelezaji wa maagano ambayo Mwenyezi Mungu alifanya nao. Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ni Mungu kweli na Mtu kweli, ni daraja na utimilifu wa ufunuo wote. Kwa njia yake, baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu zimeweza kujionesha miongoni mwa watu na uso wake kuwaangazia wote.

Ni sehemu ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Siku ya Jumatano, tarehe 16 Januari 2013. Baba Mtakatifu anasema, Neno wa Mungu ni daraja kati ya Mungu na mwanadamu, anayewawezesha waamini kuuona uso na hatimaye, kuzungumza na Mungu ambaye ni Baba yao. Kwani mtu ambaye amemwona Mwana awe na uhakika kwamba, amekwisha kumwona Baba.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika kwa namna ya pekee, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujibidisha kuuona uso wa Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Yote haya ni kwa ajili ya kuwaandaa waamini kutafakari mwanga wa Ufalme wake wa milele.

Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote heri na baraka tele, ili waweze kuangaziwa uso wa Mungu na kuwapatia wingi wa baraka zenye furaha na amani. Anawaalika vijana kujishikamanisha na Mungu, wakijitahidi kutolea ushuhuda wa ile furaha inayobubujika kutoka katika Injili.

Amewakumbusha kwamba, tarehe 17 Januari, ya kila Mwaka, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Siku kuu ya Mtakatifu Anthonio Abate; Mmonaki, Baba wa maisha ya kiroho na kielelezo makini cha maisha ya Kikristo. Mfano wa maisha yake, uwasaidie vijana kumfuasa Kristo bila ya kujibakiza; awafariji wagonjwa wote na kuwawezesha wanandoa wapya kujenga na kuimarisha moyo wa Sala na Ibada.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika Wakristo wote kushiriki kikamilifu katika Sala na Tafakari kwa ajili ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, litakalozinduliwa hapo tarehe 18 Januari na kuhitimishwa hapo tarehe 25 Januari, Siku kuu ya Kuongoka kwa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa. Kauli mbiu inayoongoza Sala ya kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2013 ni "kile ambacho Bwana anataka kutoka kwetu": ni kutenda haki, kupenda rehema na kwenda kwa unyenyekevu.

Baba Mtakatifu anasema, hii ni sehemu ya Kitabu cha Nabii Mika, sura ya 6: 6-8. Anawaalika Wakristo wote kuwa wadumifu katika kuombea umoja wa Wakristo. Nguvu ya Roho Mtakatifu iwahamasishe kujikita katika mchakato wa kweli wa umoja wa Wakristo, ili kwa pamoja waweze kuungama kwamba, Yesu ni Mkombozi wa Dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.