2013-01-15 07:20:04

Wanafunzi shuhudieni uwepo wa Mungu kati yenu kwa njia toba na wongofu wa ndani!


Kadiri muda unavyozidi kuchanja mbuga, ndivyo tumaini na furaha ya Noeli inavyoweza kutoweka kama ndoto ya mchana, kiasi cha kusahau kwamba, Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ndiye aliyekuwa ni sababu na kiini cha furaha na matumaini kwa watu wake. RealAudioMP3

Itakumbukwa kwamba, wanafunzi wa taasisi na vyuo vikuu mjini Roma, walikianza kipindi cha Majilio kwa kusali Masifu na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, tukio ambalo kwa wanafunzi wengi limeendelea kuwa ni kumbu kumbu rejea katika maisha yao ya kiroho.

Ndivyo anavyoandika Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi wa Jimbo kuu la Roma, anapowaandikia wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vilivyoko mjini Roma, kama salam na matashi mema kwa Mwaka 2013. Anawakumbusha kwamba, macho ya Mtoto Yesu yanaendelea bado kuwaangalia na kuwafariji katika hija ya maisha yao kama wanafunzi. Kama wanafunzi, daima kuna kundi la watu linalowaangalia, kila mtu akiwa na sababu yake, kiasi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, wanachunguzwa.

Lakini, Askofu msaidizi Leuzzi anasema kwamba, hii ni alama inayoonesha kwamba, katika Jamii watu wanapenda kuangaliwa na kukaziwa macho, ili kutambua uwepo wao na kujisikia kwamba, wao pia wamo, ingawa hawavumi! Kama hakuna anayemwangalia mwingine, hapo baadhi ya watu hujisikia wanyonge na kwamba, si mali kitu! Hii ndiyo ajabu ya ulimwengu mamboleo. Ni kishawishi cha kutaka kuonekana na kutambulikana kwamba upo!!! Hakuna sababu yoyote ya msingi inayoweza kuhalalisha mantiki hii, bali ni mtu kutaka kutambulika.

Hii ni changamoto na mwaliko kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kufungua macho na kutambua uwepo wa Mungu kati yao na kwamba, Mtoto Yesu anahitaji kupendwa na kuthaminiwa, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayoonesha toba na wongofu wa ndani. Vijana watambue kwamba, wanapendwa na Mungu na wao wanapaswa pia kuwa ni sadaka na zawadi kwa jirani zao. Anawaonya kwamba, wasiende kutafuta elimu ili waonekane kwamba, “wamekanyaga umande na kila mtu anapaswa kuwavulia kofia kila mahali anapopita!

Bali vijana watambue kwamba, ni zawadi safi kwa ajili yao na jirani zao. Wachakarike kusoma, ili kuwahudumia jirani zao kwa akili na moyo wao wote, wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa wachumba, wapendane na kuthaminiana kwa kutambua pia kwamba, upendo huo ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Mungu na jirani. Muda huu uwe ni fursa ya kufahamu kwamba, wewe ni zawadi na unapendwa na Mungu tangu milele, changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani zako.

Hakuna sababu ya kuogopa na kufunga macho wala kuukimbia ukweli! Simama kidete kuukabili ukweli kwa macho makavu, kwa kutambua upendo wa Mungu unaomwezesha kijana kutembea katika mwanga wa utulivu, furaha na amani, kwani anafahamu kwamba, kwa hakika anapendwa na Mwenyezi Mungu hata katika dunia hii ambayo imekuwa kama tambara bovu!

Wanafunzi wajenge utamaduni wa mshikamano wa upendo, wakitambua kwamba wao ni viumbe wapya wanaofanya hija ya pamoja. Wauanze Mwaka 2013 wakiwa na tumaini ndani mwao kwamba, wao ni zawadi safi kutoka kwa Mungu na kuwa Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatazama kwa jicho la upendo thabiti! Ndivyo Askofu msaidizi Lorenzo Leuzzi wa Jimbo kuu la Roma anavyohitimisha barua yake kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu mjini Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.