2013-01-15 12:01:38

Askofu Desiderius Rwoma ateuliwa kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jimbo la Singida sasa liko wazi!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amekubali ombi la Askofu Nestori Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba, kung'atuka kutoka madarakani na badala yake amemchagua Askofu Desiderius M. Rwoma wa Jimbo Katoliki Singida, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania.

Kwa sasa Jimbo Katoliki Singida, liko wazi. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Askofu Desiderius Rwoma kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Singida.

Askofu Rwoma, alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1947, Jimboni Bukoba. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapadrishwa kunako tarehe 28 Julai 1974. Kwa miaka mingi alikuwa ni Gombera wa Seminari Ndogo ya Rubya na Makamu Askofu jimbo Katoliki Bukoba.

Tarehe 19 Aprili 1999 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, kufuatia kifo cha Askofu Bernard Mabula. Akawekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam hapo tarehe 11 Julai 1999, Kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida.







All the contents on this site are copyrighted ©.