2013-01-14 09:17:45

Ubatizo wa Yesu ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu unaojionesha katika Fumbo la Umwilisho na Pasaka


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, hapo tarehe 13 Januari 2013, amesema kwamba, Shereha za Ubatizo wa Bwana, zinafunga rasmi shamra shamra za maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, kilichotoa mwanga unaofukuza giza la dhambi na ujinga. Kanisa katika Sherehe za Ubatizo wa Bwana linamtafakari Yesu wana wa Bikira Maria, ambaye Kanisa lilifanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Umwilisho wakati wa Siku kuu ya Noeli.

Katika Siku hii, Kanisa linakutana na Yesu akiwa mtu zima, akipokea Ubatizo wa Toba Mtoni Yordani na kwa njia ya Ubatizo wake, akayatakatifuza maji yote duniani, kama Liturujia ya Mashariki inavyokazia.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Yesu Kristo alikwenda kupata Ubatizo wa Toba, ni kielelezo cha mwanzo wa utume wa maisha yake ya hadhara, yanayojionesha kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Umwilisho, pale Mwenyezi Mungu alipoamua kujinyenyekesha na kushuka kutoka mbinguni, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Kwa ufupi kabisa, hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu unaojionesha kwa namna ya ajabu kwa njia ya uwepo wa Yesu Kristo miongoni mwa watu. Yesu alipokea Ubatizo wa Toba kama kielelezo cha mshikamano na binadamu, ndiyo maana Yohane alipomwona anakuja, akawaambia wanafunzi wake, tazameni Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia.

Yesu alipobatizwa, mbingu na nchi zilifunguka na Roho Mtakatifu akamshukia kwa mfano wa Njiwa na sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu ninayependwa naye, msikieni Yeye”. Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utekelezaji wa utashi na mapenzi ya Mungu katika maisha yake, yanayoonesha upendo unaofikia hitimisho lake katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Yesu ni kielelezo cha maisha ya mtu mpya, ambaye katika sura ya ulimwengu huu anaamua kuchagua njia ya unyenyekevu na uwajibikaji makini, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake, ili kusimama kidete kutangaza Ukweli na Haki.

Baba Mtakatifu anasema, kuwa Mkristo ni changamoto ya kujitahidi kuishi katika mtazamo huu, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Ubatizo, mwamini amezaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na kwamba, Kanisa limepewa dhamana ya kuwakirimia watu upya wa maisha, changamoto ya kukataa dhambi na nafasi zake, ili kushikamana na Kristo; ni mwaliko wa kumkataa Shetani kwa kumtambua Kristo kuwa ni Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, katika Maadhimisho ya Sherehe ya Ubatizo wa Bwana, amebahatika kuwabatiza watoto ishirini waliokuwa na umri kati ya miezi mitatu hadi minne. Kwa namna ya pekee, ametuma salam na matashi mema kwa watoto wote waliozaliwa katika kipindi hiki na anawaalika wakristo kutambua dhamana waliyojitwalia wakati walipopokea sakramenti ya Ubatizo, inayowawezesha kuanza hija ya maisha ya uzima wa milele. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kila mwamini anachangamotishwa kutambua ile zawadi ya Ubatizo, inayoonesha upendo wa Mungu na kwamba, kwa njia hii waamini wanakuwa kweli ni watoto wa Mungu

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alikumbusha kwamba, Jumapili, tarehe 13 Januari, 2013, Mama Kanisa ameadhimisha Siku ya 99 ya wakimbizi na wahamiaji duniani, iliyoongozwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Imani na Matumaini”. Kwani wale wanaohama katika nchi zao wanakuwa na imani na matumaini kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi; wanafanya hivyo kwa vile wana mtumainia Mwenyezi Mungu anayeongoza mapito ya maisha yao, kama alivyofanya kwa Mzee Ibrahim, Baba wa Imani. Wahamiaji na wakimbizi ni watu wenye imani na matumaini thabiti.

Baba Mtakatifu amezikumbuka Jumuiya za Wahamiaji wa Kikatoliki walioko mjini Roma na kuwaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Watakatifu Frances Cabrini na Mwenyeheri Giovanni Battista Scalabrini.








All the contents on this site are copyrighted ©.