2013-01-14 09:13:02

Ubatizo wa Bwana ni kielelezo cha hali ya juu kabisa ya unyenyekevu unaopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Sherehe za Ubatizo wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Januari 2013, Kwenye Kikanisa na Sistina, alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga ishirini, kielelezo cha kazi ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulitajirisha Kanisa kwa watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu, tayari kuanza maisha mapya na kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya Waamini.

Ubatizo wa Bwana ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu wa Kristo katika kutekeleza Mpango wa Kazi ya Ukombozi, kwa njia ya utii hata kifo cha aibu pale juu Msalabani. Yesu anaanza maisha yake ya hadhara kwa kupewa Ubatizo wa toba na wongofu wa ndani kutoka kwa Yohane Mbatizaji. Mtakatifu wa Mungu na ambaye hakuwa na doa la dhambi, anaonesha mshikamano wa dhati na wadhambi, ili kutambua umuhimu wa kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, kwa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani, ili kumrudia Mungu kwa moyo na akili zote.

Yesu anaonesha ukaribu wake kwa mwanadamu, ili kutoa changamoto ya kuondokana na ubinafsi na dhambi, ili hatimaye, kumpokea na kumkubali Kristo katika maisha, ili aweze kuwanyanyua na kuwapeleka kwa Baba yake wa mbinguni. Huu ni mshikamano wa dhati uliomwezesha Kristo kuzama kabisa katika undani wa maisha ya mwanadamu katika mambo yote, isipokuwa hakuwa na dhambi. Aliuonja udhaifu wa mwili wa mwanadamu, akamwonea huruma na kukubali kuteseka pamoja naye, ili kumpatia fursa ya kutubu. Kazi ya Ukombozi iliyokamilishwa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, inapania kuganga wale waliopondeka moyo, kuwafariji wagonjwa pamoja na kuwaondolea dhambi zao.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, Ubatizo wa Bwana ni kitendo cha unyenyekevu na upendo mkuu unaoonesha ile furaha ya ndani inayodhihirisha mshikamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu, linaloonesha kwamba, Yesu Kristo ni Masiha, aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni ili kuwakomboa watu wake kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti; kwa njia ya Fumbo la Msalaba, linaloonesha ile nguvu ya Mungu inayomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi. Yesu anatekeleza yote haya kama Mchungaji mwema anayeyamimina maisha yake, ili kuwakirimia waja wake uzima wa milele na hivyo kuwapatanisha na Baba yake wa Mbinguni. Ni kwa njia ya Ufufuko kutoka katika wafu kwamba, mwanadamu anakombolewa kutoka katika mauti na ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi unaonekana wazi.

Baba Mtakatifu anasema, watoto waliobatizwa wanaungana na Yesu katika Fumbo la Pasaka, chemchemi ya maisha mapya, ili kuweza kushiriki katika Ufufuko wake kwa kuzaliwa tena upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, ili kuwa kweli ni watoto wateule wa Mungu wenye uwezo wa kumwita Mungu, Abba, yaani Baba! Watoto waliobatizwa wameondolewa dhambi ya asili na sasa ni sehemu ya watoto wa Kanisa, changamoto ya kuishi kwa ukamilifu wito wao wa kuwa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupata uzima wa milele wanaokirimiwa kwa njia ya Ufufuko wa Kristo.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wazazi wa watoto waliobatizwa kwamba, kwa kuwaombea watoto wao Ubatizo, wanaonesha imani na furaha ya kuwa Wakristo na mawe hai katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni furaha ya kujitambua kwamba wao kweli ni watoto wa Mungu, wanaokumbatia upendo wa Mungu na ile furaha ya kuungana na Kristo ndiyo inayowaongoza katika hija ya maisha yao kwani Yeye ni kiini cha maana ya maisha yao. Ni mwanzo wa maisha ya imani yanayojengeka kwa kumfahamu na kujenga urafiki wa dhati na Kristo, unaompatia mwanadamu uhuru kamili.

Baba Mtakatifu anawaambia Wazazi wa Ubatizo kwamba, wanayo dhamana nyeti inayowataka kuwasaidia wazazi wa watoto waliobatizwa katika malezi, kwa kurithisha kweli za kiimani sanjari na kutolea ushuhuda wa tunu za Kiinjili, ili kuwajengea watoto hawa nafasi ya kuimarisha uhusiano wao na Kristo, kwa njia ya mifano bora ya maisha na utekelezaji wa fadhila za Kikristo katika maisha yao, kwa kusimama kidete pasi ya kulegeza kamba! Baadhi ya watu ndani ya Jamii wanadhani kwamba, wale wanaoishi imani yao kwa ukamilifu ni watu waliopitwa na wakati! Hata miongoni mwa Wakristo kuna wale wanaodhani kwamba, uhusiano wao na Kristo ni kizingiti cha uhuru binafsi. Lakini, jambo hili si kweli!

Mwelekeo huu ni finyu kwani hautambui uhusiano uliopo na Mwenyezi Mungu katika hija ya imani, unajionesha katika nguvu ya upendo wa Kristo, unaomwondoa mwanadamu kutoka katika ubinafsi wake na kuwawezesha kujenga mshikamano wa dhati na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, kwani Mungu ni upendo. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya Kikristo inayojionesha pia katika sura ya mwanadamu na hatima yake.

Maji ya Ubatizo yaliyobarikiwa kwa Ishala ya Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya maisha mapya inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayewajalia uwezo wa kuwa kweli ni watoto wake wapendwa. Watoto hao kwa njia ya Roho Mtakatifu wamejaliwa fadhila za kimungu; yaani: imani, matumaini na mapendo. Fadhila hizi hazina budi kurutubishwa kwa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, ili kufikia ukomavu utakaomwezesha mwamini kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaweka watoto waliobatizwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza katika kila hatua ya maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.