2013-01-14 10:13:37

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yalenge kupyaisha na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake


Askofu Josè Camnate na Bissign wa Jimbo Katoliki la Bissau nchini Guinea Bissau katika barua yake kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Jamii wanamoishi. Ni mwaliko wa kuimarisha imani katika hija ya maisha ya kikristo kwa kuhakikisha kwamba, imani hii inakuwa ni tendaji kama njia ya kushuhudia kile wanachoungama kwa midomo na akili zao. RealAudioMP3

Kutokana na watu kukata tamaa na wasi wasi wa kuporomoka misingi ya haki na amani, kuna haja kwa waamini kushikamana kwa pamoja, ili kukabiliana na magumu pamoja na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao kama waamini na kama Jamii ya watu wa Guinea Bissau. Mwaka wa Imani, uwawezeshe waamini kutambua fadhila za kimungu katika maisha yao na kujitahidi kuzimwilisha kama njia ya ushuhuda amini.

Watu wengi wanakabiliwa na ukosefu wa kinga za kiroho mwilini kutokana na kumezwa mno na malimwengu, kumbe, kugundua fadhila ya imani ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuitolea ushuhuda katika matendo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Guinea Bissau.

Anasema, haitoshi kubatizwa na kupewa jina la kikristo au kushiriki katika Ibada na Maadhimisho mbali mbali ya Liturujia ya Kanisa, bali imani inayoungamwa, adhimishwa, mwilishwa na kusaliwa, ijioneshe katika vipaumbele vya waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani. Imani iguse medani mbali mbali za maisha.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujikita katika majiundo makini ya awali na endelevu, ili kuifahamu imani yao inayopata chimbuko katika Maandiko Matakatifu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Waamini washiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, bila kusahau kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu katika safari ya maisha yake ya kiroho.

Waamini watambue na kuthamini tunu msingi na fadhila za maisha ya ndoa na familia za Kikristo, wawe tayari kuzitetea kwa hali na mali. Waguswe na mahangaiko ya jirani zao kwa kuwaonjesha Injili ya Upendo. Mwaka wa Imani ni kipindi cha neema na mwaliko wa kuimarisha Imani katika matendo; matumaini kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuimarisha upendo na mshikamano wa dhati miongoni mwa wafuasi wa Kristo na waamini wa dini nyingine kwa njia ya majadiliano ya kiekumene na kidini, ili wote kwa pamoja, waweze kujisikia kuwa ni watoto wa Mungu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wawaonjeshe jirani zao, ile furaha ya imani kwa Kristo na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.