2013-01-11 13:14:52

Wabunge wa Kenya wajiongezea marupurupu kibao kabla ya kuvunjwa kwa Bunge!


Kabla ya wananchi wa Kenya hawajarejea tena kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi, 2013, Wabunge wa Kenya wameamua kujiongezea marupurupu zaidi, yatakayoigharimu Serikali ya Kenya kiasi cha shilingi billioni mbili, watakapokuwa wanahitimisha shughuli zao Bungeni. Katika muswada huo wa sheria, wabunge wanataka wapewe hati za kusafiria zenye hadhi ya kibalozi, usalama wao pamoja na kupewa mazishi ya kitaifa.

Wananchi wengi wa Kenya wanauangalia muswada huu kwa jicho la makengeza, wakati wanasubiri kama utapishiwa na Rais Mwai Kibaki ili uweze kuwa ni sheria. Katika muswada huo, Rais wa Kenya baada ya kumaliza utumishi wake, atakabidhiwa kitita cha jumla ya shilingi za Kenya millioni 12.6. Baadhi ya wananchi wa Kenya waliohojiwa wanasema kwamba, katika muswada huu Wabunge wameshindwa kuonesha uzalendo kwa nchi yao na badala yake wamejizamisha katika uchu wa mali na heshima, ingawa baadhi yao wanaendelea kushutumiwa kwamba ni mafisadi, wala rushwa na wazembe.

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga anasema, Wabunge wanapaswa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa wananchi waliowapigia kura badala ya kujiingiza katika tamaa ya kupenda fedha mno, inayoweza kuhatarisha amani, usalama na ustawi wa nchi. Hata baada ya kung'atuka madarakani bado wabunge wanataka wapewe ulinzi? Baadhi ya wananchi wanaendelea kuhoji! Wamesahau kwamba, kuna watu wasiokuwa na hatia nchini Kenya wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama! Lakini wao, jambo hili wanalifumbia macho na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masilahi yao binafsi.







All the contents on this site are copyrighted ©.