Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Alhamisi, Januari 10, 2013, amekamilisha
ziara yake yenye mafanikio makubwa katika Mkoa wa Tabora kwa kuweka jiwe la msingi
la Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Tabora. Katika kitendo chake cha kuhitimisha
ziara yake ya siku tano Mkoani humo, Rais Kikwete ameungana na mamia ya wananchi wakiongozwa
na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, kwenye sherehe za kuweka jiwe
la msingi kwenye Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja huo unaogharimiwa na Benki
ya Dunia na Serikali ya Tanzania.
Uwanja wa Tabora ni moja ya viwanja vitatu
vya ndege ambavyo vinatengenezwa upya na kupanuliwa katika Mradi unaogharimu Sh. Bilioni
45 zilizotolewa na Benki ya Dunia na Sh. Bilioni tisa zilizotolewa na Serikali ya
Tanzania. Mbali ya Tabora, viwanja vingine kwenye Mradi huo ni Uwanja wa Ndege wa
Bukoba na Uwanja wa Ndege wa Kigoma.
Akizungumza kwenye sherehe hizo, Mheshimiwa
Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa mbali na mkopo huo wa Benki ya Dunia, Wizara
yake pia inaendesha Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Sumbawanga
na Shinyanga na uwekaji taa za kuongozea ndege kwenye Uwanja wa Tabora. Mradi huo
unagharimiwa kwa mkopo wa Sh. Bilioni 100 kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – European
Investment Bank.
Uwanja wa Tabora unakaratabiwa na kupanuliwa kwa awamu tatu.
Katika awamu ya kwanza itajengwa njia ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami
kwa urefu wa mita 1,900 na upana wa mita 30. Hii itawezesha ndege zenye uwezo wa kubeba
abiria 70 kutua kwenye Uwanja huo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bwana Omar Chambo
amemwambia Rais Kikwete kuwa katika awamu ya pili, litajengwa eneo la maegesho ya
ndege lenye uwezo wa kuegesha ndege tatu kwa wakati mmoja na kujenga kwa jengo la
kisasa la abiria na mizigo pamoja na kujenga kiungio (taxiway). Amesema kuwa katika
awamu ya tatu itajengwa njia ya pili ya kurukia na kutua ndege kwa kiwango cha lami.
Aidha, Serikali imepanga kujenga kituo kikubwa cha hali ya hewa ambacho kitakuwa moja
ya vituo vikubwa zaidi vya hali ya hewa katika Afrika.
Ujenzi wa awamu ya kwanza
unafanywa na Kampuni ya Sino Hydro kutoka China na unasimamiwa na mhandisi mshauri
M/S SSI Engineers na Environmental Consultant kutoka Afrika Kusini akishirikiana na
kampuni za Howard Humphrey na Nosuto Consultants za Tanzania na Netherlands Airports
Consultants. Rais Kikwete amepanda ndege hapo hapo uwanjani Tabora mara baada ya kukamilika
kwa sherehe hiyo kurejea Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania
imetangaza hatua kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa abiria na mizigo, ikiwa ni
pamoja na ununuzi wa mabehewa na injini za treni, katika hatua kubwa za aina yake
kuchukuliwa na Serikali kwa muda mrefu katika kurekebisha usafiri wa treni nchini.
Waziri
wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo Alhamisi,
Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa
Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yenye mafanikio makubwa
ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia
Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uwekaji jiwe
hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza kubadilisha reli nyepesi,
iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya Kati. Amesema kuwa kwa kupitia mashirika
yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya marekebisho hayo
makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa mashirika hayo tayari wamefika
Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia
Wizara yake na mashirika yake hayo, imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza
mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza
mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika. Katika namna
inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini, Mheshimiwa
Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia imeagiza crane mpya na kubwa
ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia kilo 100.
Kuhusu injini za treni, Waziri
Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing)
injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje
ya nchi. Pia Waziri amesema kuwa oda imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini
mpya 13 za treni ambazo malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama
utengenezaji wa injini hizo utaanza.
Aidha, Waziri amesema kuwa Wizara kupitia
mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza kufanya ukarabati mkubwa
wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa nchini. “Mheshimiwa Rais, kwa hesabu
nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na injini kiasi cha 26 ambazo
zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe
amemwambia Rais Kikwete.