Mshikamano wa kimataifa katika maboresho ya huduma ya elimu, afya ba maji safi na
salama nchini Haiti!
Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, katika utafiti wake, lina
bainisha kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu tangu tetemeko la ardhi lilipotokea
nchini Haiti, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika huduma kwa watoto hasa katika
sekta ya elimu, afya na lishe.
Idadi ya watoto wenye umri wa miaka sita hadi
kumi na mmoja, wanaosoma shule za msingi wanaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na
kwamba, vifo vya watoto wachanga chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia ishirini,
kati ya Mwaka 2005 hadi mwaka 2012. Juhudi hizi zimepelekea pia udhibiti mkubwa wa
magonjwa ya milipuko kama vile Kipindupindu na kuhara yaliyokuwa yanasababisha vifo
vingi vya watoto nchini Haiti. Maboresho ya huduma bora ya maji safi na salama yanaendelea
kwenye Kambi za watu wasiokuwa na makazi maalum.
Hizi ni juhudi zinazoonesha
ushirikiano wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na wadau mbali mbali wanaounganisha nguvu,
rasilimali fedha na watu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Haiti ambao waliathirika
vibaya sana kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba nchi yao katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita na hivyo kupelekea maafa makubwa nchini humo.