2013-01-11 08:21:58

Kanisa kama Familia ya Mungu inayowajibika


Tafakari Zaburi 128 (127):
Hii ni zaburi ya hekima, watunzi wa kundi hili kwa njia ya kurudiarudia ujumbe na maonyo wanataka kugongomelea katika akili za wasilizaji wao hofu ya Mungu kwani yenyewe inamzawadia mtu ustawi na furaha. Zaburi hii inazungumza na mmoja ambaye ni mwanafamilia na mkulima. Anaambiwa juu ya baraka tatu ambazo Mungu anamnyeshea juu yake kama ataenda kulingana na imani yake: atafurahia amani kamilifu kwa kupata mavuno ya kutosha ya kazi yake, atapata watoto wengi na ustawi wa Jiji la Yerusalemu akiwa na maisha marefu.

Mababa wa Sinodi ya Afrika, walipenda kulieleza Kanisa la Bara letu, kuwa ni ‘Familia.’ Mzaburi anatusihi kuwa na familia yenye amani, twapaswa kuwa wachamungu na kupenda kufanyakazi. Hii ni tafakari nzuri kwa Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika.

Neno hofu, kwa Kiebranina Yare, linatumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu. Mbele ya Mungu, wachamungu walitambua kwamba wako mbali sana na Muumba wao. Kwao Mungu ni wa tofauti kabisa. Kwa mtazamo huu, hofu ni jambo jema. Kutokana na Mungu kuwa kwao fumbo; ndiko kulikozaa heshima na uchaji kwa Yeye aliyetofauti kabisa. Hofu hii haisababishi uchungu wa moyo, yanayoambatana na hasira. Ni kinyume chake, ni chemchemi ya Baraka na heri: Heri mtu amwogopaye Bwana, aendaye katika njia yake.

Taabu ya mikono yako hakika utaila, utakuwa na heri, na kwako kwema. Kwa mkulima yeyote wa eneo ambalo ni jangwa na lenye mvua haba. Baraka hii ilikuwa na maana kubwa katika maisha yake. Kwa mlengwa wa tungo hii hali ilikuwa mbaya zaidi, licha ya ubaya wa ardhi na hali mbaya ya hewa, kulikuwapo na kunyonywa na bughudha toka kwa wageni waliokuwa wakiwatawala. Kwa hakika kila mmoja wetu anapaswa kuheshimu na kupenda kazi za mikono; hasa vijana. Hekima ya wahenga inatuambia ukicheza ujanani, utalipa uzeeni. Uvivu ni kumkufuru Mungu aliyetupa ardhi na mito kwa ajili ya ustawi wetu.

Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako. Hii si kauli ngeni kwa watu wa Mashariki. Ni desturi kwa wao kupanda mzabibu kando ya nyumba, ili kutumia vizuri ardhi kwani ilikuwa haba, ni jangwa na majabari, na pia kuufanya mti huo upate jua. Ulitumika kupendezesha mazingira ya nyumba, lakini pia kuulinda dhidi ya wezi. Hivyo, mzabibu huu mzuri, wenye matunda mengi, ulikuwa ni nembo ya akina mama wengi wa Mashariki. Kuwa na watoto wengi ni baraka kubwa kwa taifa la Mungu (soma Mwa 15:5). Usasa usiwe kikwazo kwa sisi kukacha kuzaa, na kuwafanya wanyama: mbwa, paka kuwa
ndio watoto wetu!

Wanao kama miche ya mizeituni, wakiizunguka meza yako: huu ni umithilisho mzuri sana; kuna mti wa mzabibu mkongwe na umeanza kupukutika, umezungukwa na miche mingi mizuri na yenye nguvu, ambayo imechipuka toka katika shina hili kongwe. Miche hii yaonekana ikilitegemeza, kulilinda na kulikumbatia shinda kongwe. Kwa hakika hata mavuno hayajapungua licha ya ukongwe wa shina msingi, kutokana na uzao wa miche hii mipya. Ndivyo mtunzi wetu anavyomithilisha watoto wema na wenye upendo kwa baba yao mchamungu. Kila mche unachangia katika wema wa wote. Hii ni baraka kubwa
kwa mzazi yeyote yule.

Bwana akubariki toka Sayuni; uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. Kuwa na ustawi ndani ya familia yako, si mwisho wa kuwajibika kwako. Mkulima wetu anaambiwa afungue macho yake na kuona patakatifu pake. Kwani hapo ndipo ilipo chemchemi ya heri zote alizonazo. Hata sisi leo, mafanikio yetu yasitutenge na Kanisa, iwe ni kushiriki katika jumuiya au katika ujenzi wa kanisa; toka Yerusalemu ndipo baraka za Mungu zinatushukia.

Kwa hakika: Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana. Si kwa fedha au tanzanite, lakini ya heri isiyochakachuliwa na tufani za maisha. Kwani Bwana atakuwa mlinzi wake daima.








All the contents on this site are copyrighted ©.