2013-01-10 10:02:41

Zaidi ya watu 150 wamekwisha poteza maisha katika mapigano ya kikabila nchini Kenya


Chama cha Msalama Mwekundu Kimataifa nchini Kenya, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kinasema kwamba, kuna watu kumi wamefariki dunia baada mapigano ya kikabila yaliyotokea kwenye Wilaya ya Mto Tana, usiku wa kuamkia Alhamisi, tarehe 10 Januari 2013.

Kuna idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa katika mapigano hayo ambayo tangu mwei Agosti 2012 yamekwisha pelekea watu zaidi 150 kupoteza maisha. Mapigano ya kikabila kati ya kabila la Orma na Pokomo yanatokana na kugombania ardhi kwa ajili ya kilimo na kulishia mifugo. Baadhi ya wachungu wa mambo ya kisiasa wanasema pengine kuna mkono wa wanasiasa wakati huu Kenya inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013.

Hivi karibuni, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya aliitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina, ili kubainisha sababu za chokochoko za kikabila zinazopelekea watu wasiokuwa na hatia kupoteza maisha yao, ili kujenga misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.