Utapimlo mkali unatishia maisha ya watoto zaidi ya 200,000 nchini Sudan ya Kusini
Licha ya maboresho ya huduma ya afya ya Mama na Mtoto sehemu mbali mbali za dunia,
lakini bado kuna idadi kubwa ya watoto wanaopoteza maisha yao Barani Afrika kutokana
na utapiamlo wa kutisha. Hii inatokana na kuendelea kuwepo kwa ukame wa mda mrefu
uliopelekea baa la njaa linalochochea pia umaskini.
Taarifa zinabainisha kwamba,
kuna watoto laki mbili nchini Sudan ya Kusini wanaokabiliwa na utapimlo wa kutisha
na kwamba, kila siku watoto wenye uzito mdogo wanaendelea kupata tiba kwenye Hospitali
kuu ya Juba, inayotoa huduma pekee kwa watoto. Kila mwaka Jumuiya ya Kimataifa inajitahidi
kuwahudumia watoto wapatao sabini elfu, lakini hali ni mbaya zaidi Sudan ya Kusini
kwa idadi ya watoto wenye utapiamlo wa kutisha imefikia laki mbili. Hali ni mbaya
zaidi vijijini ambako watoto wanaendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa homa
kali na Malaria.
Takwinu za Idadi ya Watu nchini Sudan ya Kusini zinaonesha
kwamba, kuna jumla ya watu millioni tisa na nusu ya idadi ya wananchi wa Sudani ya
Kusini ni vijana na watoto. Itakumbukwa kwamba, Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake
kunako Mwaka 2011 baada ya kupiga kura ya maoni, iliyoonesha kwamba, wananchi wa Sudan
ya Kusini walikuwa wanataka kujitenga na Sudan Kongwe. Kwa bahati mbaya, Serikali
ya Sudan ya Kusini bado iko katika mchakato wa maboresho ya miundo mbinu iliyokuwa
imeharibiwa vibaya kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Serikali
kwa kushirikiana na wadau mbali mbali inaendelea kupambana na baa la umaskini, linaloendelea
kupungua siku hadi siku, lakini tatizo la utapimlo bado ni kubwa miongoni mwa watoto
kutoka Sudan ya Kusini.