2013-01-09 08:15:43

Tanzania imepania kupunguza uhaba wa walimu wa shule za Serikali kwa mwaka 2013


Serikali ya Tanzania itaajiri na kusambaza walimu 28,746 katika shule za msingi na sekondari kuanzia mwezi huu wa Januari 2013, hatua ambayo itapunguza kwa zaidi ya nusu ukosefu wa walimu katika shule za Serikali nchini. Mpaka sasa Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo Serikali inasema kuwa italimaliza katika miaka michache ijayo kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbali mbali nchini.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza mjini Igunga siku ya Jumatatu, Januari 7, 2013 kuwa kati ya walimu hao watakaoajiriwa na kusambazwa 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu. Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu kwenye siku ya pili ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Tabora, Rais Kikwete amesema kuwa mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.
Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee ikiwa inahitaji kiasi cha walimu 285. Hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo la ukosefu wa walimu nchini ambalo kwa namna moja linachangia matatizo ya elimu nchini.
Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379 walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246 walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu. Wakati shule za Serikali nchini zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi nchini zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459 hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.
Rais Kikwete amewaambia wananchi kuwa Serikali pia inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi. Rais Kikwete pia amezungumzia suala la huduma ya maji nchini akisema kuwa Serikali yake imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbali mbali ya Tanzania.
Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete amesema kuwa kufuatia kuzinduliwa kwa Mradi wa Maji wa Bulenya mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70. Ameahidi kuwa asilimia 30 iliyobakia itapatiwa majawabu na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambayo yatavutwa kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa miji ya Nzega, Igunga na Tabora na vijiji ambako mabomba ya mradi huo yatapitia.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, Januari 7, 2013, ameweka jiwe na msingi kwenye ujenzi wa daraja kubwa na kuzindua mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Tabora ambako anafanya ziara ya kikazi ya siku nne kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi ya maendeleo.
Katika tukio ambalo ni la kihistoria tokea Tanzania kupata uhuru, Rais Kikwete ameanzisha rasmi ujenzi wa daraja kwenye Mto Mbutu, nje kidogo tu ya mji wa Igunga, kwa kuweka jiwe la msingi la daraja ambalo litatoa huduma kwa wakazi wa mikoa ya Tabora, Singida, Shinyanga na Simiyu.
Wakati Rais akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Daraja hilo katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa mji wa Igunga na vijiji vya jirani, wananchi waliendelea kuvuka Mto huo uliojaa maji kutokana na mvua zinazoendelea sasa Mkoani Tabora kwa kutumia miguu wengi wakiwa wamebeba baiskeli, pikipiki, mifugo na mali zao nyingine vichwani mwao kuelekea mjini Igunga kwenye masoko.
Ujenzi wa Daraja la Mbutu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na ahadi ya Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huo ambako aliahidi kuwa Serikali yake ingejenga daraja kwenye Mto huo ambao huhamahama kutegemea wingi wa maji.
Daraja hilo litawanufaisha moja kwa moja wakazi 84,000 wa kata saba za Mkoa wa Tabora na wakazi wa wilaya jirani za Iramba (Mkoa wa Singida), Meatu (Mkoa wa Simiyu) na Kishapu (Mkoa wa Shinyanga) na mzungumzaji mmoja baada ya mwingine katika sherehe hizo ameelezea ujenzi wa daraja hilo kuwa ni ukombozi mkubwa wa wananchi wa eneo hilo. Inakadiriwa kuwa ujenzi wa daraja hilo utakamilika Novemba mwaka huu na utagharimu kiasi cha Sh. bilioni 11.286 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Rais Kikwete pia amezindua Mradi wa Maji na Chujio la Maji la Mji wa Igunga katika kijiji cha Bulenya, nje kidogo ya Mji huo wa Igunga. Mradi huo uliogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 6.7 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania utawanufaisha wakazi wa Mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo ambao wakazi wake sasa wataweza kupata maji kwa asilimia 70. Kiasi cha watu 32,600 watanufaika na maji ya mradi huo ambao sasa watakuwa wanapata lita 2,600 za maji kwa siku badala ya lita 710 za sasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.