2013-01-09 10:28:16

Kanisa linatafuta kwanza kabisa mafao ya wengi, haki, amani na maendeleo endelevu!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hotuba ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, inalenga matashi mema katika mchakato wa kufahamiana, kati ya wawakilishi wa Nchi na Mashirika ya Kimataifa pamoja na Vatican.

Kardinali Bertone, anabainisha kwamba, Vatican katika utume na shughuli zake za kidiplomasia inalenga zaidi katika kulinda na kudumisha maendeleo endelevu yanayokumbatia mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika hotuba yake ameonesha wasi wasi na vipaumbele ambavyo viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kuvifanyia kazi, katika harakati za ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu duniani, dhidi ya: vita, kinzani, chuki na uhasama ambao unaendelea kushika kasi ya ajabu sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa amekazia kwa namna ya pekee haki na amani; kwa kusema kwamba, mchakato wa ujenzi wa amani ya kweli unaanza kwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu. Lakini kwa bahati mbaya haki hizi zimekuwa pia ni chanzo cha kutoelewana miongoni mwa Jamii.

Kardinali Bertone anasema kwamba, kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha; kuwa na mikakati pamoja na sera makini zinazopania maboresho ya maisha ya watu na wala si uchumi unaotafuta faida kubwa hata kwa gharama ya maisha ya watu! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Dhamana na mchango wa Familia katika Jamii hauwezi kamwe kupuuzwa. Familia zinapaswa kutekeleza wajibu wake wa kutoa elimu na kuchagua shule ambazo watoto wao wataweza kupata malezi na majiundo makini kadiri ya utashi wao. Familia zina jukumu ya kutoa malezi bora kwa ajili ya Jamii nzima.

Wajenzi wa amani anasema Kardinali Tarcisio Bertone hawana budi kutambua na kuheshimu wajibu wa dini na taasisi zake katika kuchangia mafao ya wengi ndani ya Jamii. Serikali zitambue na kuthamini mchango wa dini katika maendeleo na ustawi wa watu wake na wala si kuziona dini na taasisi zake kama kikwazo cha maendeleo. Viongozi wa dini wahamasishe misingi ya haki, amani na utulivu.







All the contents on this site are copyrighted ©.