Jengeni utamaduni wa kuandika vitabu kutunza historia ya watu wenu!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amezindua kitabu cha historia ya kabila la Wapimbwe
lililoko mkoani Katavi na kutayataka makabila mengine kuandika historia zao ili waweze
kutunza kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizindua kitabu hicho hivi
karibuni mjini Mpanda, Waziri Mkuu aliwataka watu wa makabila mengine ya mkoa wa Katavi
ambayo ni Waruira, Wabende, Wakonongo na Warungwa wafanye tafiti kuhusu mila na tamaduni
zao na kisha waandike vitabu vyao.
Kabla ya uzinduzi huo, mtunzi wa kitabu
hicho, Bw. Peter Mgawe alisema kitabu hicho kimetokana na utafiti uliofanywa tangu
mwaka 2007 ambao ulilenga kukusanya taarifa na masimulizi mbalimbali kutoka kwa wazee
wa Kipimbwe ambao wameishi miaka mingi huku wakiwa na hazina ya mila na tamaduni za
kabila hilo ambalo pia ni kabila lake Waziri Mkuu Pinda.
“Hili ni kabila dogo
lisilofahamika na wengi, nimekuwa nikitafuta taarifa na machapisho (literature) mbalimbali
kuhusu kabila hili lakini sikuwahi kupata chochote… ndipo nikamshirikisha Mheshimiwa
Waziri Mkuu juuya kufanya utafiti na kuandika historia yetu naye akalikubali wazo
langu,” alisema Bw. Mgawe ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama,
Dar es Salaam.
Akizungumza na wakazi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri Mkuu
alisema utafiti huo usiishie hapo tu, bali wafanye tafiti nyingine kuhusu mavazi,
vyakula, ndege, wanyama waliokuwa wakipendelewa na mababu zao ili kuongeza hazina
ya taarifa ya kabila hilo.
“Lengo la kitabu hiki lilikuwa ni kuhifadhi katika
maandishi historia ambayo ilikuwa imefichika ndani ya vichwa vya wazee wetu kutoka
vijiji mbalimbali vya Mpimbwe… nafurahi kwamba tunao wazee watatu waliokuwa katika
warsha ya kwanza kabisa iliyofanyika mwaka 2008. Leo hii wako hapa na wanashuhudia
matunda ya kazi yao,” alisema Waziri Mkuu.
Wazee hao ni Mzee Simba Pangani
Kalulu (76) kutoka kijiji cha Mamba, Mzee Valeri Kipande (76) kutoka kijiji cha Lyangalile
na Mzee Moses Kasalani (67) kutoka kijiji cha Mirumba. Vijiji vyote hivyo viko wilaya
ya Mlele, mkoani Katavi.