Mshikamano wa upendo na waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi na Matumaini ya Bara la Afrika
kwa siku za usoni!
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma, inaliangalia Bara la
Afrika kwa matumaini makubwa na inapenda kushirikiana na wananchi Barani Afrika katika
harakati za kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kupambana kufa na kupona na ugonjwa
wa Ukimwi, ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa ni kikwazo cha maendeleo kwa familia nyingi.
Mradi wa "The Dream" unaosimamiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio Barani Afrika
kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na utapiamlo
miongoni mwa watoto, ulioanzishwa kunako mwaka 2002 unaendelea kuonesha mafanikio
makubwa kwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa Mamamjamzito
kwenda kwa mtoto.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho
ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa Mwaka 2012, aliiomba Jumuiya ya Kimataifa, kuonesha
mshikamano wa dhati na waathirika wa Ukimwi duniani, lakini zaidi katika nchi zinazoendelea.
Uwe ni mkakati unaopania kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa Mamamjamzito
kwenda kwa mtoto, jambo ambalo linawezekana, ikiwa kama watu wataonesha mshikamano
wa upendo.
Kwa mara ya kwanza mradi wa DREAM ulianza kufanyiwa majaribio nchini
Msumbiji na sasa mradi huu umeenea nchini: Angola, Cameroon, Guinea Bissau, Kenya,
Malawi, Nigeria, DRC na Tanzania. Ni mradi ambao umeleta mabadiliko makubwa sana miongoni
mwa wagonjwa wa Ukimwi katika nchi hizi. Wanawake wamefaidika zaidi kwani wamekuwa
wakihusishwa moja kwa moja katika kuhangaikia hatima ya maisha yao wenyewe pamoja
na watoto wao, ili kuwajengea matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Kutokana
na changamoto mbali mbali zinazowakabili waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, kunako mwaka
2005, nchini Msumbiji, wanawake waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, walianzisha
Chama cha Wanawake Wenye Ndoto ya Matumaini Mapya. Mama Artemisa Chiziane ni kati
ya waasisi wa ndoto hii nchini Msumbiji. Ni Chama ambacho kimekuwa mstari wa mbele
kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, pamoja na kuwasaidia kukabiliana
na changamoto mbali mbali za maisha ya kifamilia.
Mama Chiziane anasema kwamba,
Mradi wa DREAM unajikita hasa zaidi katika kudhibiti, kuzuia na kutoa tiba kwa wagonjwa
wa Ukimwi, kwa kuzingatia utu na heshima ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Lengo ni kuunganisha harakati za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi
pamoja na kutoa tiba kwa kuwapatia waathirika vidonge vya kurefusha maisha. Haitoshi
tu kudhibiti, bali, kusaidia juhudi za kuokoa maisha ya watu yanayoendelea kupukutika
kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa wanawake wajawazito, mradi unapania pamoja
na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, wanatokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi
kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto. Ni matumaini ya mradi wa DREAM kwamba, baada ya
miaka michache ijayo, hata Barani Afrika, kunaweza kuwepo kizazi cha watoto wasioathirika
kwa virusi vya Ukimwi.
Kutokana na ushirikiano mzuri na wadau mbali mbali katika
mradi huu, watoto zaidi ya elfu kumi nchini Msumbiji wamezaliwa pasi ya kuwa na virusi
vya Ukimwi. Ndoto hii inawezekana kuwahusisha wanawake wengi zaidi, kwa kuwapatia
dawa za kurefusha maisha.
Hizi ni juhudi ambazo zinapaswa kuungwa mkono pia
na Serikali anasema Mama Artemisa Chiziane, ili kutoa matumaini kwa wanawake wengi
zaidi, hasa wale wanaoishi vijijini. Huko ni vigumu zaidi kupata dawa za kurefusha
maisha na matokeo yake, watu wengi bado wanaendeleza imani za kishirikina, mila na
desturi ambazo zimepitwa na wakati.