2013-01-08 14:39:05

Askofu mkuu Ruwaichi asema, ushemasi ni daraja la huduma ya Injili, Altare, Upendo na Huruma ya Mungu kwa Watu wake!


Daraja ya ushemasi kama vile pia daraja ya upadri na uaskofu inalenga katika kutoa huduma kwa Injili ya Kristu, Altare ya Bwana, Huruma na Upendo wa Mungu. Ujumbe huo umetolewa na Askofu Mkuu Yuda Thaddei Ruwa’ichi wa jimbo kuu la Mwanza wakati wa Misa Takatifu ya kumpa daraja ya ushemasi wa Jandokasisi Peter Madata. Misa hiyo iliadhimishwa na Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliyeongoza mapadri, watawa, na waamini walei wa Jimbo kuu la Mwanza katika kumsindikiza Shemasi huyo kupokea Neema hizo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi ameifafanua sura yote ya sita ya Mwinjili Marko ili kupata umaana kamili wa sehemu ya Injili hiyo iliyosomwa katika Misa hiyo (Rej. Marko 6, 34-44) ambapo Kristo anawaonea huruma umati wa watu waliokuwa kama Kondoo wasio na mchungaji, akawafundisha na kuwalisha mikate mitano na samaki wawili.
Mwanzo wa sura ya sita ya Marko, Kristo anafundisha na watu wanamdharau kwa kuwa wanamfahamu kama Mwana wa Seremala, na wanawafahamu maumbu zake. Kristo anafundisha, awalisha watu Neno la Mungu: mkate wa uzima ushukao toka mbinguni. Anafanya hivyo kwa upendo kwani, anafahamu njaa, kiu, umaskini, na mahangaiko ya wanadamu. Hata leo, Kristo anaendelea kujimega kwa ajili ya wengine, ili mwanadamu ampokee katika Ekaristi na katika Neno lake ili kupata uzima wa milele.
Kwa upendo huo huo, anawaita wengine ili wamsaidie kuendeleza utume wake wa kukabili njaa, kiu, mahangaiko ya watu; wawaponye, wawalishe na kuwafariji wagonjwa. Ndivyo sehemu ya pili ya sura ya sita ya Mwinjili Marko inavyosimulia uteuzi wa wale Mitume kumi na wawili. Wanaagizwa kutokujilimbikizia mali, kutokuwa na wasiwasi bali kujikabidhi mikononi mwa Mungu naye atawaongoza. Popote wanapojikuta watulie na kutekeleza mapenzi ya Mungu, wasitangetange. Kumbe, mashemasi, mapadri, na maaskofu wanaalikwa kujitosa kikamilifu, kujimega na kutimiza mapenzi ya Baba wa mbinguni. Ukasisi wa Kristo haufuatwi ili kujipatia maraha na starehe mbali mbali, bali kutumika na kujitoa sadaka hata iliyo kubwa.
Ndivyo sura ya sita ya Mwinjili Marko inavyosimulia sehemu ya tatu juu ya kukamatwa na kuuawa kwa Yohane mbatizaji. Maisha ya ukasisi na hata ya ukristo kwa ujumla yana gharama zake. Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitolea mfano wa wana ndoa ambao baada ya kuishi pamoja kwa muda hugundua kila mmoja mapungufu yake na kuanza kuhangaika nayo. Amewaalika wana ndoa pia kuvumiliana, kusaidiana na kuzingatia maagano yao ya ndoa kwa kuwa: waaminifu, kupendana na kusaidiana katika taabu na raha, katika furaha na dhiki mpaka wanapokamilisha hija ya maisha yao hapa duniani, daima wakipania kupata utakatifu.
Katika utume Makasisi na Wana wote wa Mungu wanahitaji faragha, ndivyo inavyosimulia Injili ya Marko sura ya sita. Faragha ni wakati wa kutulia, kujikusanya, kutafakari, kusikiliza Neno la Mungu katika ukimya. Tafakari na faragha katika ukimya si jambo la ziada bali la lazima na la msingi katika maisha ya Mkristo na hasa kwa watu wa daraja, alihimiza Askofu Mkuu Ruwa’ichi. Hivyo faragha inapaswa kuthaminiwa kila siku, vinginevyo Mashemasi na Mapadri watakuwa wanajikomoa wenyewe. Wao wamewekwa wakfu, basi wathamini hali hiyo ya kuwekwa wakfu.
Marko anaendelea kusimulia jinsi Kristo anavyoendelea kuwafundisha watu na kuwalisha. Hata pale wanafunzi wanapoingiwa na huruma ya woga na kumuomba awaagize makutano kutawanyika, Kristo anawaamuru “wapeni ninyi chakula”. Kristo anawaagiza wanafunzi wake kutumia rasilimali walizonazo ili kuzikabili changamoto wanazokutana nazo. Askofu Mkuu Ruwa’chi amewaagiza makasisi na waamini wote kujitahidi kutumia rasilimali chache walizo nazo ili Mungu azibariki na kuzizalisha badala ya kukata tamaa kwa upungufu wa vitu fulani. Zaidi ya hayo amewaagiza kuwa na mipango mikakati katika utendaji wao, kwani Kristo anapoagiza watu kuketishwa katika makundi, anahaimiza juu ya kuwa na utarataibu na mikakati katika utendaji.
Jandokasisi Peter Madata amepewa daraja la ushemasi wa mpito tarehe 8 Januari 2013 katika Kanisa kuu la Epifania, Bugando, Jimbo kuu la Mwanza. Naye anatarajia kupokea daraja ya Takatifu ya upadri kati ya Mwezi Julai na Septemba. Shemasi Madata alizaliwa tarehe 30 Septemba 1979 katika Kijiji cha Shishani wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Wazazi wake ni Thomas Bhujilima na Lucia Mlwisha akiwa mtoto wa pili kati ya watoto nane.
Alijiunga na mwaka wa malezi katika Nyumba ya malezi ya Mwenye heri Yohane Paulo II, Kawekamo, Mwanza mnamo 2003. Masomo ya Falsafa aliyapata katika Seminari kuu ya Mtakatifu. Anthony wa Padua, Ntungamo, Bukoba kati ya Mwaka 2004 na Mwaka 2007. Mwaka 2008 alijiunga na Seminari kuu ya Mt. Augustino, Peramiho kwa masomo ya tauhidi ambako atahitimu Juni 2013.
Askofu Mkuu Yuda Thaddei, mapadri, watawa na waamini walei Jimbo kuu la Mwanza, wanamtakia kila jema katika huduma yake ya Injili, Altare, Huruma na Upendo wa Mungu.

Na Pd. Celestin Nyanda,
Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.