2013-01-07 10:19:49

Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania wapata Mashemasi wapya wanne!


Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Jumapili tarehe 6 Januari 2013 kwenye Kikanisa cha Nyumba ya Malezi, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, ametoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Majandokasisi wanne wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.

Askofu Nyaisonga amewataka Mashemasi wapya kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema vipaji na karama mbali mbali walizojaliwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya mafao ya Kanisa, Shirika na Jamii kwa ujumla; watambue kwamba, wamepewa bure na sasa ni jukumu lao kuvitumia kikamilifu.

Akili na vipaji vyao, viwasaidie kumtafuta, kumfahamu na kumtumikia Yesu Kristo, Mwanga wa Mataifa, kama walivyofanya wale Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali. Karama hizi pia zitumike kuonesha njia ya ukweli inayojikita katika huduma kwa Familia ya Mungu. Wawasaidie waamini kulifahamu na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao; daima wakiwa mstari wa mbele kumfuasa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Kama Mashemasi wa Kanisa Katoliki watambue kwamba, ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu pamoja na Mapadre katika matendo ya huruma; huduma ya Neno la Mungu na huduma kwa Sakramenti za Kanisa kadiri ya daraja lao. Ili kuleta hamasa ya kupenda na kulitafakari Neno la Mungu, Mashemasi wapya hawana budi kujitaabisha kuandaa Tafakari ya Neno la Mungu ili iweze kuleta mguso na mvuto, hatimaye, kuzima kiu ya maisha ya kiroho. Mashemasi wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na kanuni za Kanisa.

Wawe ni wahudumu makini wanaoongozwa na ujuzi, maarifa na Neno la Mungu kama walivyokuwa Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, ili kuwasaidia watu kukutana na Yesu Kristo, Mwanga wa Mataifa na Mkombozi wa Ulimwengu. Kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu la Ushemaji, Mashemasi hao wanaanza kujiandaa kwa ajili ya kuingia kwenye Daraja Takatifu la Upadre, changamoto ya kujikana na kumfuasa Kristo bila hata ya kujibakiza katika maisha ya useja, utii na ufukara wa Kiinjili.

Mashemasi wapya waliowekwa wakfu wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana ni Alex Isengwa, Danford Mahumi, John Greyson na Raymond Kaele. Itakumbukwa kwamba, Mashemasi hawa kabla ya kupewa Daraja hili takatifu walipokewa rasmi kwenye Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye nyumba ya Malezi ya Shirika, Miyuji, Dodoma.







All the contents on this site are copyrighted ©.