2013-01-07 08:47:27

Salam, matashi mema na mikakati ya Umoja wa Afrika kwa Mwaka 2013


Dr. Nkosazana Dlamini Zuma, Kamishina wa Umoja wa Afrika, katika salam na matashi ya Mwaka Mpya 2013 anabainisha mambo kadhaa yaliyojitokeza Barani Afrika katika kipindi cha Mwaka 2012, kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu, haki na amani. Kumekuwepo na dalili za ukuaji wa uchumi Barani Afrika kwa asilimia kumi.

Baadhi ya nchi za Kiafrika zimebahatika kugundua na kuanza kuchimba utajiri mkubwa wa madini, mafuta na gesiasilia; mambao ambayo yakitumiwa kwa mafao ya wengi, yanaweza kusaidia katika harakati za maboresho ya uchumi na maisha ya Watu Barani Afrika.

Mkakati wa kuimarisha na kudumisha utawala bora unaendelea kufanyiwa kazi na Serikali mbali mbali Barani Afrika, ili kuhakikisha kwamba, haki, amani na utawala wa sheria vinazingatiwa na wote. Kuna dalili za maendeleo ya kisiasa na kiuchumi nchini Somali, ingawa bado hali yake inaendelea kubaki tete! Suluhu ya mgogoro kati ya Sudan Kongwe na Sudani ya Kusini ni hatua kubwa kwa Umoja wa Afrika, lakini pia inapaswa kuimarishwa kwa mazungumzo yanayoendelea kwa sasa kati ya viongozi wa nchi hizi mbili, ili kweli amani iweze kupatikana na watu waishi katika hali ya utulivu, wakijikita katika harakati za kujiletea maendeleo yao wenyewe baada ya vita, kinzani na migogoro ya miaka mingi.

Dr. Nkosazana Zuma anabainisha kwamba, katika mashindano ya Olympic yaliyofanyika Jijini London, wanamichezo wengi kutoka Bara la Afrika walijinyakulia ushindi hasa katika mashindano ya riadha.

Mwaka 2013 utashuhudia matukio kadhaa ya Barani Afrika. Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU unaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ulipoanzishwa, sanjari na Miaka 11 ya Umoja wa Afrika. Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya OAU ni tukio kubwa na fursa kwa Bara la Afrika kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia wapi walikotoka, mahali walipofikia pamoja na kujiwekea mikakati ya maendeleo kwa miaka ijayo. Tume ya Umoja wa Afrika inatarajiwa kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka minne yaani kuanzia Mwaka 2013 hadi Mwaka 2017.

Mwaka 2013 Bara la Afrika litafanya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Ni fursa nyingine kwa wananchi Barani Afrika kujiunga na wachezaji wao ili kushuhudia nyasi za Viwanja vya Afrika ya Kusini vikiwaka moto! Michezo ni furaha! Hapa ni mahali ambapo wachezaji wanapaswa kuonesha nidhamu ya hali ya juu, haki, ujasiri, heshima katika tofauti zao.

Waswahili wanasema, asiyekubali kushindwa huyo si mshindani. Kimsingi Kabumbu ina tabia ya kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kwa kuvuka vikwazo vya mipaka, rangi, dini, lugha na tamaduni za watu. Wakati wa michezo tofauti hizi zinafutika na watu wanajikuta wakizama kuangalia jinsi ambavyo wanasoka wanalisakata kabumbu kwa umahiri mkubwa, kila upande ukipania kupata ushindi.

Mwaka 2013 una changamoto kubwa zinazoendelea kulisubiri Bara la Afrika, hasa katika mchakato unaopania kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo ya kweli. Bado kuna migogoro ya kivita inayoendelea kufuka moshi huko DRC, Mali na Jamhuri ya Afrika ya kati. Maeneo yote haya yanahitaji umakini wa Umoja wa Afrika ambao pia unatarajia kutuma watazamaji wa kudumu katika uchaguzi mkuu nchini Kenya, unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013.

Dr. Nkosazana Dlamini Zuma anabainisha kwamba, Bara la Afrika linaendelea kucharuka katika mikakati na mipango ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hivi karibuni, Umoja wa Afrika unatarajiwa kuzindua Chuo Kikuu cha Afrika. Nchi nyingi zinaendelea kuonesha maboresho ya miundo mbinu kama njia ya kujiletea maendeleo katika nchi husika bila kusahau ushirikiano wa nchi hizi kikanda. Mbinu mkakati wa kuimarisha biashara na soko la ndani Barani Afrika unazidi kupamba moto.

Kilimo bado kinaendelea kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi Barani Afrika. Lengo kwa mwaka huu na miaka ijayo ni kukuza tija na uzalishaji, ili kuliwezesha Bara la Afrika kujitosheleza kwa chakula na kuendelea kupata ziada sanjari na kukuza mazao ya biashara ili kuinua pato na hali ya maisha ya wakulima wengi Barani Afrika. Idadi ya wakazi wa Bara la Afrika kwa sasa inakadiriwa kufikia watu zaidi ya billioni moja.

Utunzaji bora wa mazingira pamoja na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele na Umoja wa Afrika, ili kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kijacho wanarithi mazingira bora ya kuishi. Umoja wa Afrika unapania pia kuboresha afya ya Mama na Mtoto ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Bado Bara la Afrika linacghangamotishwa kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu magonjwa ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watu wengi Barani Afrika.

Takwimu zinaonesha kwamba, wanawake Barani Afrika, walau ni asilimia hamsini ya wanawake wote wanajihusisha katika shughuli za uchumi na uzalishaji mali na mchango wao unaoendelea kuonekana katika Jamii. Ni Jukumu la Umoja wa Afrika kuendelea kukazia umuhimu wa haki na fursa sawa kati ya wanawake na wanaume Barani Afrika hadi kufikia asilimia 50 kwa 50. Wanawake wanapaswa kushirikishwa katika utoaji wa maamuzi pamoja na kujifunga kibwebwe kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Dr. Nkosazana Dlamini Zuma, Kamishina wa Umoja wa Afrika anahitimisha salam na matashi mema kwa Mwaka 2013 kwa kuwashukuru viongozi wote wa nchi za Kiafrika na wananchi wa Bara la Afrika kwa kuwaunga mkono katika utekelezaji wa mikakati, majukumu na malengo ya Umoja wa Afrika. Kwa pamoja, wanalenga kukuza na kudumisha mafanikio yaliyokwishakupatikana kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Bara la Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.