Afya ya Mzee Nelson Mandela, Rais mstaafu wa Afrika ya Kusini, inaendelea kuimarika
baada ya kulazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na baadaye kupasuliwa
ili kuondoa mawe yaliyokuwa kwenye figo zake, Kwa takribani majuma matatu, Mzee Mandela
alilazwa Hopsitalini na kuruhusiwa kurudi nyumbani hapo tarehe 26 Desemba 2012.
Taarifa
ya Rais Jacob Zuma wa Afrika ya kusini, iliyotolewa Jumapili tarehe 6 Januari 2013
inabainisha kwamba, afya ya Mzee Madiba inazidi kuimarika na anaendelea kupata matibabu
akiwa nyumbani kwake nje kidogo ya Jiji la Johanesburg. Pole pole Mzee Madiba anaanza
kurudia katika hali yake ya kawaida. Rais Zuma anamhakikishia Mzee Madiba kwamba wananchi
wa Afrika ya Kusini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia
wanampenda na wanaendelea kumsindikiza kwa sala, dua na maombi yao.
Wananchi
wengi ndani na nje ya Afrika ya Kusini, walianza kuingiwa na wasi wasi kuhusu afya
ya Mzee Madiba sanjari na umri wake kuendelea kuwa mkubwa. Itakumbukwa kwamba, Mzee
Nelson Mandela ana umri wa miaka 94, si haba. Mzee Mandela alikaa kizuizini kwa kipindi
cha miaka 27 wakati wa utawala wa Ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na huko akashambuliwa
na ugonjwa wa Kifua kikuu. Akaachiwa huru mwaka 1990.
Kunako mwaka 1994 akachaguliwa
kuongoza Afrika ya Kusini, huku akipeperusha bendera ya ushindi ya ANC. Kwa mara ya
mwisho Mzee Madiba kuonekana hadharani ni wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia kwa
Mwaka 2010, wakati viwanja vya michezo Afrika ya Kusini, vilipowaka moto!