2013-01-05 09:01:43

“Tutembee kidhati tukiongozwa na mwanga wa imani ya kikristo hadi kumfikia Mungu”



Katika masimulizi ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunakutana na makundi makubwa mawili yaliyofika kumtembelea na kumwona mtoto Yesu aliyezaliwa: Kundi la kwanza ni lile la wachungaji na la pili ni la Majusi. RealAudioMP3

Lakini katika makundi haya mawili, Kanisa halijapanga siku ya pekee ya kusherekea ujio wa wachungaji walipoenda kumtembelea Mtoto Yesu, isipokuwa iko siku ya leo tunaposherekea matembezi ya hiari ya Majusi wakitokea Mashariki ya mbali hadi Betlehemu kumwona mtoto Yesu. Kwa nini tushereke matembezi ya Majusi na siyo ya wachungaji au wote wawili?

Swali hili ni dogo na la udadisi lakini jibu lake ni muhimu kwa sababu Majusi hao wanaweza kufumbua macho na kutufanya tuweze kuona vizuri mambo yahusuyo dini na imani yetu kijumla. Jibu hilo muhimu linapatikana hasa kwenye namna au jinsimakundi hayo mawili yalivyofunuliwa au yalivyopata taarifa za kuzaliwa Yesu na kuvutwa kwenda kumtembelea Mtoto Yesu.

Hebu tuanze na wachungaji. Hao walipata taarifa juu ya kuzaliwa kwa Yesu kwa kuelezwa na malaika waliowafikia usiku wa manane walipokuwa wanachunga kondoo, hatimaye malaika hao wakaimbia hata wimbo: “Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema.” Kwa hiyo wachungaji hawa walifunuliwa moja kwa moja na malaika toka angani au toka mbinguni mambo ya Kimungu.

Watu karibu wote hatuna matatizo juu ya ufunuo wa mtindo huo, yaani kuangaziwa moja kwa moja na Mungu mwenyewe au na malaika wake mambo ya mbinguni. Aidha, ufunuo wa mtindo huu unavuta watu wengi na ni rahisi sana kuufuata. Mathalani, inatosha mmoja kusema: “Nimetokewa na Mungu na nimeangaziwa dawa hii inayotibu magonjwa kadhaa”. Hapo apo watu watamiminika toka pande zote kumfuata, au “Mungu ameniambia mwakani ni mwisho wa duniani, hivi mwaka huu ni wa kujiandaa hakuna kulima.” Ndivyo ilivyotokea kwa wachungaji, “Mara moja wakaondoka na kwenda Betlehemu kumwona mtoto aliyezaliwa.”

Majusi wa mashariki ya mbali wao kumbe walijua juu ya kuzaliwa kwa Yesu kwa njia ya kuchunguza nyota. Ilibidi Majusi waitafsiri wenyewe alama hii ya huluka isiyosema. Kwa njia ya nyota waliweza kufahamu kuzaliwa kwa Yesu na kuanza matembezi ya kitambo kirefu wakiongozwa na nyota hadi kufika Betlehemu. Walifika huko wakiwa kama wapagani, wakamwabudu Yesu na kumtolea zawadi zao wakiwa kama wapagani, wakarudi tena nyumbani kwao walikotoka wakiwa bado wapagani.

Hatusikii kwamba Majusi hawa baadaye waliongokea dini ya Kiyahudi au ya Kikristo. Kumbe uabudu wao ulikubalika na Mungu, naye kwa njia ya ndoto akawaongoza vyema katika safari ya kurudi makwao walikotoka salama salimini.

Tukikumbuka kwamba, wale Majusi watatu walikuwa wapagani, watu ambao waliweza kuona mapenzi ya Kimungu kwa kusoma huluka yaani, kwa kusoma miendo ya nyota na vitu vingine vya angani, hapo unaona yale matembezi ya Majusi yanaweza kutupatia changamoto kubwa sana juu ya imani kwa Mungu waliyo nayo watu wengine wasiokuwa wa imani yetu. Kwa hiyo habari hii ya Majusi inatufumbua macho juu ya kuuelewa ukweli huu kwamba Mungu hafungwi na utamaduni wa dini yoyote ile. Kwamba katika kila dini hususani zile dini za kipagani kuna imani yenye kudokeza uwepo wa Kristu na kuwakwamba Mungu anao uhusiano pia na watu wa dini nyingine wasio Wayahudi wala Wakristo.

Aidha, katika Injili na masomo ya leo tunadokezewa njia tatu za kumtambua Mungu: Mosi, kwa njia ya Maono au ufunuo wa Kimungu; pili kwa njia ya Nyota au ufunuo wa hulaka, na tatu kwa njia ya Msaafu au Maandiko Matakatifu. Wachungaji waliokuwa wanadharauliwa kuwa wachafu, na hawakuweza kushiriki madhehebu ya kuabudu kwenye Hekalu bila kutakaswa kabla, hao wakafunuliwa moja kwa moja kwa njia ya malaika.

Majusi wao wakafunuliwa kwa njia ya kwa kusoma nyota. Wakati Waandishi wakuu wa mfalme Herodi walifahamu kwa njia ya kusoma na kupekua Maandiko Matakatifu. Hizi zote ni njia tofauti za kufikia ukweli uleule mmoja. Hata hivyo, haimaanishi kwamba kila mapokeo ya dini ni sawa na mengine. La hasha! angalia tu jinsi Mateo anavyoonesha hilo, wakati nyota ile iliyokuwa inaongoza Yerusalemu ilipowapotea, hapo Majusi ikawabidi waulize na wategemee Maandiko matakatifu yaliyowaongoza hadi kufika Bethlehemu. Yaani, licha ya mwanga wa nyota uliowaongoza, Majusi walihitaji pia mwanga wa pekee wa Maandiko matakatifu ili kuwafikisha kwa Yesu.

Swali la msingi linabaki palepale linatusumbua: Ni nani aliyeenda kumwona Yesu? Herode na Waandishi wake waliobobea katika kujua Maandishi Matakatifu walishindwa kwenda kumwona mtoto Yesu, bali Majusi waliokuwa wanafuata mwanga wa nyota walifanikiwa kwenda. Kwa nini? Kwa sababu wakuu wa kiyahudi hata kama walikuwa na ukweli ulioangazwa na Maandiko, hawakuyafuata, yaani hawakuwa wanatembea kadiri ya mwanga wa Maandiko hayo.

Majusi, kumbe waliokuwa wanaangalia nyota, waliweza kuifuata na ikawaongoza. Suala la msingi hapa siyo kuujua ukweli, bali ni jinsi tunavyotembea na kuufuata mwanga wa ukweli huo tulio nao. Kwa hiyo, ni bora kuwa na mwanga mdogo kama ule wa nyota iliyowaongoza Majusi, kuliko kuwa na mwanga mkali wa Misahafu Mitukufu na wa Maandiko Matakatifu halafu kutoyafuata.

Watu wa Agano la Kale, wayahudi waliamini kwamba wao ndiyo waliokuwa Taifa pekee la Mungu. Wakaugawa ulimwengu katika makundi mawili: Kundi la Wayahudi waliokuwa Taifa la Mungu na Wapagani ambao hawakuwa Taifa la Mungu. Baadhi ya manabii wao na watu wenye hekima walijaribu sana kusahihisha imani yao hiyo kwa kuwaelewesha kwamba upendo wa Mungu ni kwa watu wote. Jambo hilo lakini halikuwa wazi na halikuzama ndani ya vichwa vyao hadi alipofika Yesu Kristo.

Ndivyo inavyotueleza barua kwa Waefeso kwamba, Yesu aliyaunganisha makundi yote mawili, Wayahudi na Wapagani kuwa kundi moja na kuvunjilia mbali ukuta ule wa chuki na uaduni uliokuwa unawatenganisha (Waef. 2:14). Hii ni habari njema ambayo ambao Paulo aliagizwa kuihubiri: “yaani Wapagani wamepata kuwa warithi wa ufuasi, sehemu moja ya mwili, na warithi wa ahadi za Yesu Kristu kwa njia ya Injili” (Waef. 3:6).

Somo la pili linaibua ukweli huo ulio kama fumbo: “fumbo likapata kujulikana kwangu kwa njia ya ufunuo” (Waef. 3:3). Ni fumbo kwa hoja mbili: Mosi, akili ya mtu peke yake isingeweza kufikia kutambua ufunulio huo”; pili, hata baada ya ukweli huo kufunuliwa, bado inaonekana kuwa ni fumbo na utata kwa akili ya binadamu. Ni utata na fumbo bado katika imani ya kikristu tunaosadiki, kwa upande mmoja, kwamba Wayahudi ni Taifa teule la Mungu, na kwa upande mwingine ni kwamba “Mungu hana upendeleo, na kwamba kila mtu wa kila taifa anayemtambua na kumwabudu na kufanya kitu kilicho chema na kinachostahiki haki, anakubalika naye” (Mdo 10:34-35).

Wakristu wa kanisa la awali walielekea kufanya kosa hilohilo kama Wayahudi wa zamani, kwa kudai kwamba nje ya kanisa hakuna wokovu. Mtaguso wa Vat. II ukatufumbua macho, ukafungua madirisha ili Roho Mtakatifu wa Mungu aingine, na tukaja kutambua kwamba ukweli juu ya Mungu uko hata kwa watu wa dini nyingine, ingawaje si kwa kiwango hichohicho kama kilivyo katika Kanisa.

Wakristo, tunasadiki kwamba dini yetu inao ukweli wote wa imani. Na ni vyema kusadiki hivyo. Lakini imani hiyo inatusaidia nini endapo hatutembei katika ukweli huo? Wapagani au wasiosadiki wanaofuata mwanga hafifu wa hoja za kihuluka wanaweza kufika kwa Yesu kabla ya Wakristo walio na ukweli wa juu kabisa uliofunuliwa na Mungu lakini kumbe hawatembei katika imani hiyo.

Hii ndiyo changamoto ya ukweli tunaosherekea leo katika habari hii ya Majusi hawa wapagani wanaomtafuta na kumkuta Bwana. Kuna Mungu mmoja tu kwa wote wanaomtafuta kwa imani na kwa moyo mnyofu na kuongozwa kwake, hata kama wanamwita kwa majina tofauti. Kitu kimoja ambacho Wakristo wanacho cha pamoja na dini nyingine ni hiki kwamba wote tunamwabudu Mungu huyohuyo mmoja.

Sisi sote ni watoto wa Mungu huyo mmoja. Kwa baadhi lakini, wanaona vigumu sana kuutambua, kuupokea na kuuthamini ukweli huo, kwa vile watu wote ulimwenguni wanaelekea kuona kwamba wao wenyewe peke yao ndiyo wawezao kumkaribia Mungu na kuwa na ukweli wote juu ya Mungu.

Hata hivyo, tofauti kati ya imani ya Kikristo na imani ya dini nyingine, haipo katika kule kuwa na ukweli wa Mungu, bali ni kule kwamba Mungu kwa njia ya ufunuo pekee katika Kristo, tunaweza kuona ukweli wa Mungu kwa uwazi zaidi, na kufuata njia za Mungu kwa karibu zaidi katika maisha yetu ya kila siku. Kwa hiyo jambo la kuzingatia na la kukumbuka daima ni hili kwamba kama tunalala usingizi, na kupumzika tu “mtama wa mama waliwa na ndege,” hata kama tuko katika njia na nafasi nzuri ya kumtambua Mungu kwa njia ya Kristo, watu wengine ambao hawako katika njia nzuri wanaweza kututangulia na kulifikia lengo kabla yetu.

Hebu leo tulitafakari Fumbo hilo tunaposherekea sikukuu ya Majusi waliofika toka nchi za kipagani kumwabudu mtoto Yesu, pindi “Taifa teule” la Mungu kule Yerusalemu walikuwa wamelala hawana habari kwamba ufalme wa Mungu umefika. Tutembee kidhati tukiongozwa na mwanga wa iamni ili tukafike aliko Muumba wetu.
Heri kwa Siku kuu ya Epifania.

Tafakari hii imeandaliwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.