2013-01-05 14:46:58

Tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya Tanzania kuanza kukusanya maoni ya katiba kutoka katika Makundi, Changieni vyema kwa mafao ya Taifa la Tanzania


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya 2013 na kuzungumzia mchakato wa Katiba unaoendelea na kusema Rais hapaswi kulalamikiwa kwani yote aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo l Jumamosi, Januari 5, 2013 katika mkutano wake na Waandishi wa Habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika tarehe 19 Desemba mwaka 2012.

“Kuna kitu gani kipya alichosema Rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mimi katika mikutano yangu yote nanyi nimeyaeleza na hakuna asiyejua,” alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. “Rais alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu, kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni…haya yote yapo kwenye sheria ambayo Wabunge waliipitisha,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la Mwandishi wa Habari mmoja aliyetaka kujua kauli ya Tume kuhusu maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa Rais aliingilia kazi za Tume.

“Hivi ingekuwaje kama Rais angetoa salam za Mwaka Mpya bila kuzungumzia mchakato muhimu kwa nchi kama huu wa Katiba,” alihoji Jaji Warioba. Akizungumzia mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba alisema kazi ya kukusanya maoni ilianza tarehe 2 Julai mwaka jana na Tume yake imetembelea na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria mikutano hiyo na kati yao, wananchi 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza katika mikutano na wengine 253,486 walitoa maoni yao kwa maandishi katika mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba, takwimu hizi hazijumuishi maoni yanayoendelea kukusanywa na Tume yake kupitia posta, totuvi ya Tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi kufikia Ijumaa, Januari 4, 2013 jumla ya ‘sms’ 16,261. Kuhusu idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao, Mwenyekiti huyo alisema Tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa kilichokuwa kinatafutwa na Tume ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa kupiga kura.

“Ilikuwa ni muhimu kufikia watu wengi iwezekanavyo na ndiyo maana tumefika kila sehemu. Lakini tangu awali, tulishasema hatutaweza kumfikia kila mtu,” alisema na kuongeza kuwa Tume yake imeridhika na idadi na maoni yaliyotolewa na wananchi na kutoa mfano wa Tume ya Nyalali ambayo alisema ilipokea maoni ya wananchi 21,000 lakini Ripoti ya Tume hiyo ilisheheni mambo muhimu kwa taifa.

Jaji Warioba alifafanua kuwa katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni, wananchi wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala, haki, maadili na mamlaka yao na mengineyo. Aliongeza kuwa mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ililelenga kupata hoja za msingi ili Tume iweze kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa katika mikutano ya Mabaraza ya katiba itakayofanyika kila wilaya.

Akizungumzia hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa kuanzia Jumatatu, tarehe 7 Januari, 2013, Tume hiyo itaanza kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya. Makundi hayo ni Vyama vya Siasa; Vyama vya Kitaaluma; Asasi za Kiraia; Taasisi za Kidini, Vyama vya Wafanyakazi, Wakulima na Wafanyabiashara na makundi mengine mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume yake imeshawasiliana na makundi hayo na imeandaa utaratibu wa kukutana na wawakilishi wao katika ofisi za Tume na baadhi ya kumbi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi Mei 2 mwaka jana (2012) na kazi ya kukusanya maoni kupitia mikutano imefanyakika kwa awamu nne. Awamu ya kwanza ilifanyika kati ya Julai 2 – 30, 2012 wakati awamu ya pili ilifanyika kuanzia tarehe 27 Agosti – 28 Septemba, 2012. Awamu ya tatu iliyofanyika kati ya terehe 8 Oktoba, 2012 na tarehe 6 Novemba, 2012 na awamu ya nne na ya mwisho ilifanyika kati ya tarehe 19 Novemba – 19 Desemba mwaka jana (2012).









All the contents on this site are copyrighted ©.