Maandamano makubwa kupamba viunga vya Mji wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Siku
kuu ya Epifania
Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana katika viunga vya mji wa Vatican, yatapambwa
na maandamano ya umati mkubwa wa wasanii kutoka mjini Arezzo na vitongoji vyake, wakiwa
wamevalia mavazi ya kijadi watapita katika barabara kadhaa za mji wa Roma hadi kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ambako watashiriki katika Sala ya Mchana.
Maandamano haya ni kielelezo cha amani, mshikamano na udugu miongoni mwa Jumuiya ya
watu wanaoishi mjini Roma na vitongoji vyake.
Mara baada ya Sala ya Malaika
wa Bwana, Mamajusi watatu watakwenda kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, ili kumpatia zawadi ya Kalisi tatu za madini ya fedha, kazi ya mikono ya
wasanii kutoka Arezzo, kama sehemu ya mchango wao katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Ni mwaka unaopania
kukuza na kuimarisha: Imani, Matumaini na Mapendo: fadhila zinazopata hitimisho lake
katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Maandamano haya yanafanya
rejea ya Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walioongozwa na nyota hadi mjini Bethlehemu
walikokwenda kumwona na kumtolea zawadi ya: dhahabu, uvumba na manemane. Wataalam
wa Maandiko Matakatifu wanabainisha kwamba: Dhahabu ni alama ya Ufalme wa Kristo:
Uvumba ni kielelezo cha Utakatifu na Umungu wa Kristo na Manemane ni alama ya ubinadamu
wa Kristo unaoashilia: mateso, kifo na ufufuko wake.