2013-01-04 07:41:06

Uwepo wa Yesu Kristo kati ya watu wake, ulete faraja, mwanga na matumaini kwa wote wanaoelemewa na Msalaba wa Maisha!


Kardinali Cormac Murphy O’Connor wa Jimbo kuu la Westminster, Uingereza, katika tafakari yake ya kipindi hiki cha Noeli anabainisha kwamba, kila mwanadamu ana Msalaba fulani katika maisha yake. Unaweza kuwa ni msalaba wa magonjwa, huzuni na simanzi; mateso na mahangaiko ya roho na mwili. RealAudioMP3

Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli yanawakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake mkuu amefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuweza kuwakirimia upatanisho, mwanga na matumaini mapya. Amekuja kuwasaidia watu kufua mapanga, mikuki na mishale ili yawe ni majembe yatakomwezesha mwanadamu kupata mahitaji yake ya msingi; mateso na mahangaiko ya mwanadamu yageuzwe kuwa ni chemchemi ya baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Watu wakumbatiane na kupeana busu la amani, linalobubujika kutoka katika uwepo wa Kristo miongoni mwao, wakikumbushana kwamba, kwa hakika, Kristo amezaliwa tena kati yao! Huyu ndiye Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi! Kuzaliwa kwa Kristo kunaleta matumaini mapya kwa watu waliochoka na kuboreka na hija ya maisha yao hapa duniani kutokana na sababu mbali mbali.

Kardinali O’Connor anasema, unaweza kuamua kuua kundi la watu, lakini huwezi kuwabusu wote kwa kwakati mmoja; busu la amani, upendo na mshikamano linalotolewa kwa mtu mmoja mmoja.

Kipindi cha Maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, iwe ni fursa ya kuchuchumalia toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli: Noeli iwasukume waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni faraja kwa wote wanaoteseka na kusononeka katika maisha yao; wanaotafuta amani na upatanisho, ili kweli utukufu wa Mungu uweze kuonekana duniani na utu wa mwanadamu uweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na wengi.








All the contents on this site are copyrighted ©.