Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2013
Ninakuleteeni kwa furaha ujumbe wa Neno la Mungu tunapoadhimisha sherehe ya Epifania
ambayo huadhimishwa kila terehe 6 Januari katika kipindi cha Noeli. Ni sherehe ambayo
Mfalme Masiha anajitambulisha wazi kwa ulimwengu.
Ni kwa njia
ya nyota, Mamajusi wanaweza kufika mahali alipokuwa na wakaweza kumsujudia na kumpatia
zawadi zao. Kumbe Yesu Kristo Masiha ni nyota inayaangaza na kuongoza maisha yetu
mpaka mwisho wa nyakati hadi kufika mbinguni.
Katika somo la kwanza tunaona
jambo la ajabu na zuri likitokea. Nabii Isaya yuko katika ndoto anaona Yerusalemu
iliyokuwa imeharibiwa kwa sababu ya vita na mapigano mbalimbali miaka 600 hivi kabla
ya Kristo sasa inakuwa chanzo cha nuru, na utukufu wa Mungu unaonekana juu yake. Mataifa
wakiwakilishwa na Mamajusi wanaijia nuru hiyo. Nabii Isaya anaimba akisema “inua macho
yako Yerusalemu utazame pande zote za dunia, wote wanakusanyana; wanakujia wewe” Ni
wimbo wa sifa kwa Yerusalemu, ni kielelezo cha kuzaliwa Masiha na kwamba atakuwa nuru
angavu kwa ulimwengu na mataifa yote watakusanyika kumsujudia na kumtolea zawadi.
Habari na uaguzi huu tunauona vema katika Injili ambapo tunawaona Mamajusi
wakitokea pande zote za dunia kwa ajili ya kuja na kumsujudia Bwana aliyezaliwa na
zaidi sana aliye nyota ya mataifa, nyota ya milele. Kwenye jumuiya zetu kunapotokea
tatizo tunaweza kulitazama kama nabii Isaya? Tutafakari.
Katika somo la pili
Mtume Paulo anapowaandikia Waefeso anawaambia juu ya kufunuliwa siri za Mungu kwa
njia ya mitume. Anasema ni kwa njia ya manabii na mitume na si wanadamu katika vizazi
vingine Mungu amefunua siri yake. Hata hivyo pamoja na kupewa siri hiyo bado mataifa
mengine wanashiriki pamoja nasi ahadi ya Bwana ya kurithi ufalme wake. Hivi neno la
Mungu linatualika kutambua kuwa sisi sote tuliobatizwa na kupokea mataji matakatifu
tumeshirikishwa katika ukoo wa kikuhani kwa ajili wokovu wetu na wokovu wa ulimwengu.
Katika
somo la Injili tunapata kuona ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya Mamajusi, wamefika
kwa mfalme Herode na wanamwuliza yuko wapi mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota
yake mashariki nasi tumekuja kumsujudia. Herode anashangaa kwa kufadhaika na anauliza
habari kwa wakuu wa makuhani na waandishi Kristu azaliwa wapi? Wanamjibu Betlehemu.
Anawaagiza Mamajusi wakati wakishamwona wamletee habari ili naye akamsujudie! Mamajusi
hawa wanaongozwa na nyota mpaka pale alipo mtoto na hawatarudi kwa Herode kwa sababu
Herode anayonia ya kutaka kumwua Mwana wa Mungu.
Mamajusi wako katika msingi
uleule wa nabii Isaya anaposema Yerusalemu ikiangaza watu wote watakuja na kumiminika
katika mji. Kumbe Mamajusi wanatimiza ule uaguzi wa nabii Isaya, wanaleta manemane,
dhahabu na uvumba. Mamajusi ni kiwakilishi cha watu wote wanaokubali kuongozwa na
ujumbe wa amani, ujumbe wa Yesu Kristu Masiha yaani nyota, nuru ya ulimwengu. Ni alama
ya kanisa lililo jumuiya ya watu wenye chimbuko moja yaani Mungu, lakini lugha, tamaduni,
umri, kabila tofauti. Watu hawa wote wako mbele ya nyota angavu ndiye Mkombozi aliyezaliwa.
Mpendwa,
unaalikwa basi leo na Neno la Mungu kujiweka chini ya maongozi ya Nyota angavu, nyota
ya milele ndani ya kanisa familia ya Mungu. Ninakutakieni heri na baraka za Mungu,ukazidi
kuongozwa na Kristu mwenyewe, daima ukampe hazina stahili kama Mamajusi kwa sifa na
utukufu wa Mungu na pia kwa wokovu wako. Heri na baraka kwa wale walio na majina ya
Epifania na majina ya Mamajusi yaani Gaspar, Melkiori na Barthazari. Mkakomae katika
kusujudu na kumtolea Mungu vipaji vyenu kama kielelezo cha kuongozwa naye katika maisha
yenu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya
C.PP.S.