Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati wa Siku kuu ya Epifania atawaweka wakfu Maaskofu
wakuu wateule!
Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican anabainisha
kwamba, Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, maarufu kama
Epifania anatumia fursa hii pia kutangaza “Mbiu ya Pasaka” inayoonesha jinsi ambavyo
Kanisa litaendelea kumtangaza na kumwonesha Kristo miongoni mwa Mataifa katika maadhimisho
mbali mbali yatakayofanywa na Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2013. Ikumbukwe kwamba,
kazi ya ukombozi inafikia kilele chake katika Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo
na ufufuko wa Kristo, unaopania kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi
na mauti. Tukio la Mamajusi kutoka Mashariki waliongozwa na nyota kwenda Bethlehemu
kumwona Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa ni tukio la kwanza kabisa linaloonesha Ufunuo
wa Bwana kwa watu wa Mataifa katika ulimwengu. Yesu Kristo ni mwanga wa mataifa na
kilele cha historia ya maisha ya mwanadamu; Yeye ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega;
Nyakati zote ni zake. Yesu Kristo ndiye anayeongoza hija ya maisha ya mwanadamu inayohitimishwa
kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake mbinguni. Monsinyo Marini anasema,
ndiyo maana katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, Kanisa linatangaza “Mbiu
ya Pasaka” inayopembua matukio makuu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Kanisa mintarafu Historia
ya Ukombozi inayojikita katika Siku kuu tatu muhimu katika maisha na utume wa Kristo:
Mateso, kifo na ufufuko wake: Jumaa kuu. Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo
la Bwana, hapo tarehe 6 Januari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa
kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu wapya wanne nao ni: Monsinyo Vincenzo Zani, Katibu mkuu
wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki; Monsinyo Fortunatus Nwachukwu aliyeteuliwa
kuwa Balozi wa Vatican nchini Nicaragua; Monsinyo Nicolas Thevenin aliyeteuliwa kuwa
Balozi wa Vatican pamoja na Monsinyo Georg Ganswein, katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, aliyeteuliwa pia kuwa ni Mkuu wa Nyumba ya Kipapa. Katika
Ibada hii, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kusaidiwa na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Kardinali Zenon Grocholewski. Maaskofu
wakuu wateule watatambulishwa kwa Baba Mtakatifu na Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti
wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.