2013-01-03 08:38:17

Wakristo 400 waimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara Jimboni Dodoma


Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, Tanzania, hapo tarehe Mosi, Januari 2013 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo mia nne, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Parokia ya Kiwanja cha Ndege. Katika mahubiri yake, Askofu Nyaisonga amewakumbusha waamini hao kwamba, wameimarishwa kwa mapaji ya Roho Mtakatifu sasa wanatumwa ulimwenguni na katika mazingira yao kutolea ushuhuda wa imani yao katika matendo.

Wakumbuke kwamba, wamepokea Sakramenti hii wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani, changamoto kwao kuifahamu, kuiungama, kuimwilisha na kuisali, kama wanavyoelekezwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Mwaka wa Imani, usaidie kuleta mabadiliko katika hija ya waamini Jimboni Dodoma, kwa kuanza maisha mapya yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, Mwanga wa Mataifa na hivyo wanachangamotishwa hata wao kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya matendo yao.

Wajikite katika toba na wongofu wa ndani, ili kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu waweze kuutakatifuza ulimwengu uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Wasimame kidete katika misingi ya imani na maisha adili, tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika mapambazuko ya Mwaka 2013.

Nchini Tanzania katika kipindi cha Mwaka 2012 kumekuwepo na kinzani za kidini na matukio ambayo yanaashilia kumong’onyoka kwa msingi wa haki, amani na utulivu, kumbe, waamini wanapaswa kuwa makini na choko choko hizi ambazo ni hatari kwa ustawi na maendeleo endelevu ya watanzania: kiroho na kimwili.

Kwa vile wameimarisha kwa nguvu na mapaji ya Roho Mtakatifu, basi waamini hawa wanapaswa kuwa mashahidi amini wa Imani ya Kanisa Katoliki, tayari kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kila mwamini atekeleze wajibu na dhamana yake ndani ya Kanisa kama kielelezo cha imani tendaji.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Padre Sostenes Luyembe, Makamu Askofu Jimbo Katoliki Dodoma, upande wa watawa, anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake, uliowawezesha hata kuuchungulia Mwaka Mpya wa 2013.

Uwe ni mwaka unaowahamasisha waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Mafanikio, matatizo na changamoto mbali mbali zilizojitokeza wakati wa safari ya Mwaka 2012 iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini, pasi ya kukata tama. Waamini na wote wenye mapenzi mema, waendelee kujenga utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa; daima wakijitahidi kuheshimu na kuthamini utu wa kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wajifunze kuwamegea jirani zao upendo unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, kama sehemu ya kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao.









All the contents on this site are copyrighted ©.