Vijana wa Taizè waanza hija ya kiroho Istanbul ili kushiriki Siku kuu ya Tokeo la
Bwana, hapo tarehe 6 Januari 2013
Baada ya Vijana wa Kiekumene wa Taizè kuhitimisha mkutano wa thelarhini na tano wa
sala mjini Roma, hapo tarehe 2 Januari 2013; tarehe 3 Januari 2013 wameanza hija ya
kiekumene, ili kumtembelea Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la
Costantinopoli inayowapatia fursa ya kushiriki pia katika Maadhimisho ya Siku kuu
ya Tokeo la Bwana, yaani Epifania hapo tarehe 6 Januari 2013 nchini Uturuki. Hiki
ni kikundi cha vijana mia moja kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaokwenda huko
ili kusali pamoja na Waamini wa Kanisa la Kiorthodox.
Kwa mara ya kwanza viongozi
wa Jumuiya ya Taizè walianza kuwasiliana na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli
mwishoni mwa mwaka 1960 na mwezi Februari 1962 Fra Roger alimtembelea na kusali pamoja
na Patriaki Atenagora wa Istanbul. Tangu wakati huo, viongozi mbali mbali wamekuwa
wakiwatembelea viongozi wa Kanisa la Kiorthodox ili kuimarisha majadiliano ya kiekumene.
Kunako
Mwaka 2005 Fra Roger na Fra Alois walimtembelea Patriaki Bartolomeo na kuoneshwa kuvutwa
sana na mikutano ya sala ya vijana inayoendeshwa na Jumuiya ya Taizè, kielelezo makini
cha jitihada za kutaka kujenga na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Baadhi ya familia
za Kikristo mjini Istanbul zimejitolea kutoa hifadhi kwa vijana hao wakati huu wanaposhiriki
pamoja nao Maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana.